FAQs

SWALI: Kwa nini Sheria ya Maadili ya Viongozi ilitungwa?

 

JIBU: Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilitungwa mwaka 1995 ili kudhibiti tabia na mienendo ya viongozi wa umma. Hii ni kufuatia kukosekana kwa kwa chombo/sheria ya kusimamia maadili ya viongozi wa umma tangu mwaka 1992 baada ya kufutwa kwa  Sheria ya Kamati ya Kusimamia utekelezaji wa Miiko ya Viongozi ya mwaka 1973 kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa. Viongozi wakawa hawazingatii tena uadilifu hivyo likatolewa pendekezo la kutungwa kwa sheria ambayo itasimamia maadili ya viongozi wa umma.

 

 1. SWALI: Je, ni kina nani walihusika kutunga sheria hiyo na Je, wananchi walihusishwa vipi katika mchakato huo?

 

JIBU: Chombo chenye mamlaka ya kutunga sheria ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bunge kupitia wabunge wake ndio walihusika katika kutunga sheria hiyo na wananchi waliwakilishwa na wabunge wao.

 

 1. SWALI: Je, Ofisi ya Maadili inawajibika vipi kwa wale Wabunge wanaotoa lugha chafu bungeni?

 

JIBU:  Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

 

 1. SWALI: Ofisi ya Maadili imewahi kuchukua hatua gani kwa viongozi wanaokiuka maadili. Mfano wa viongozi watatu ambao wamewahi kuwajibishwa na Ofisi ya Maadili?

 

JIBU:  Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

 

 1. SWALI: Ni viongozi gani wanahusika na Sheria ya Maadili?

 

JIBU:  Orodha ya viongozi wa umma imeainishwa katika kifungu 4(1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Aidha, Mhe. Rais ameongeza orodha ya viongozi mwaka 2013.

 

 1. SWALI: Wabunge na madiwani na viongozi wengine wanaochaguliwa na wananchi huwa wanaingia madarakani wakiwa wanaifahamu Sheria ya Maadili kabla au baada ya kupata madaraka?.

 

JIBU:  Kila mwananchi anapaswa kuijua Sheria ya Maadili si lazima awe kiongozi. Kwa viongozi wa umma Ofisi ya Maadili huwa inatoa mafunzo kwa viongozi wanapochaguliwa au kuteuliwa ili kuwaeleza misingi ya maadili na mipaka ya utendaji kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

 

 1. SWALI: Kuna umuhimu wowote wa wananchi kujua Sheria ya Maadili na kama upo wanaipataje Sheria hiyo?

 

JIBU:  Kila mwananchi anatakiwa kuifahamu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Kwa kuifahamu Sheria hiyo wataisaidia Ofisi kwa kutoa taarifa za ukiukwaji wa maadili unaofanywa na viongozi mbali mbali. Wananchi wanaweza kupata elimu ya maadili kupitia njia mbali mbali  kama vile redio, semina na matukio ya kitaifa ambayo yanakusanya watu wengi kwa pamoja kwa mfano maadhimisho ya sherehe za wakulima nchini(nanenane) ambapo Ofisi ya Maadili huwa inatoa elimu kwa umma katika banda la maadili. Elimu inatolewa pia kupitia kipindi cha redio na kipindi maalum cha maadili kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) siku ya Jumatatu na Star tv siku ya Jumanne kuanzia saa moja kamili hadi saa moja na nusu jioni. Hivyo, wananchi wanashauriwa wafuatilie ili kujifunza zaidi majukumu ya ofisi yetu.

 

 1. SWALI: Je, utekelezaji wa maadili unazingatia ngazi ipi?

Utekelezaji wa Sheria ya Maadili unafuata Orodha ya viongozi wa Umma ambayo imeainishwa katika kifungu 4(1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Aidha, Mhe. Rais ameongeza orodha ya viongozi mwaka 2013.

 

 1. SWALI: Kiongozi akikiuka maadili ya viongozi wa umma mwananchi ataenda kumshtaki sehemu gani?

 

JIBU:  Wananchi wanatakiwa kupeleka malalamiko yao katika ofisi za maadili zilizopo Tabora mjini, mtaa wa Jamhuri, jengo la NSSF, ghorofa ya pili. Hapo mwananchi atasikilizwa lalamiko lake bila kutozwa gharama yoyote ile na hatua zitachukuliwa. Aidha, mlalamikaji halazimiki kutaja jina lake na taarifa zake huwa ni siri kati ya mwananchi na Ofisi ya Maadili. Malalamiko yanaweza kuwasilishwa kwa njia ya simu, barua, ana kwa ana. Baada ya kupokelewa malalamiko hayo hufanyiwa uchuguzi na ikibainika kama kweli kuna ukiukwaji wa maadili, kiongozi husika hushtakiwa kwenye Baraza la Maadili na kuhojiwa kutokana na tuhuma za ukiukaji wa maadili zinazomkabili, kisha Baraza hutoa mapendekezo na mapendekezo hayo hupelekwa kwa Rais kwa hatua zaidi. Kwa viongozi ambao hawaguswi na Sheria ya Maadili, kwa mfano watendaji wa kata na vijiji wao wanawajibika kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa na Wilaya husika. Sheria inamuwajibisha Mkurugenzi ili awawajibishe watendaji wake wa chini kama mtendaji wa kijiji kata na mtaa.

 

 1. SWALI: Je, Ofisi ya Maadili inawashughulikia vipi Watendaji wa Kata na Vijiji pale wanapoomba rushwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi?

 

JIBU: Uvunjifu wa maadili kwa kiasi kikubwa unatokana na viongozi kuwa na mgongano wa maslahi yaani kutanguliza maslahi binafsi badala ya kutanguliza maslahi ya umma. Pindi, wananchi wanapokumbana na viongozi wa aina hiyo wasisite kufika katika Ofisi za Maadili kutoa taarifa kuhusu viongozi wa aina hiyo. Hakuna kiongozi ambaye yuko juu ya sheria. Mtendaji Kata au Kijiji analipwa mshahara ambao unatokana na kodi za wananchi hapaswi kumtoza pesa kwa ajili ya kupewa huduma. Wananchi nao waondokane na dhana kuwa huwezi kupewa huduma hadi utoe rushwa.

 

 1. SWALI: Je, Ofisi ya Maadili inashirikiana na TAKUKURU katika kushughulikia masuala ya rushwa?

 

JIBU: Ofisi ya Maadili haifanyi kazi kama kisiwa. Inashirikiana na ofisi nyingine kama vile ofisi ya RPC, RPO, Mkuu wa Mkoa na ofisi nyingine katika kutekeleza majukumu mbali mbali. Kwa kuwa rushwa ni moja ya vitendo vya ukiukaji wa maadili, Ofisi ya Maadili hushirikiana na TAKUKURU kwa ajili ya kukamata viongozi wanaojihusuisha na rushwa.

 

 1. SWALI: Je, msemo kuwa watunga sheria ndio wavunja sheria una ukweli wowote?

 

JIBU: Sheria zipo na zinatakiwa kufuatwa, isipokuwa wananchi wanalalamika tu bila kupeleka malalamiko yao katika ofisi husika kama Ofisi za Maadili. Cha msingi wananchi wanatakiwa kupeleka malalamiko ya viongozi mbali mbali wanaokiuka maadili kwa kuwa wao ndio wako karibu na viongozi hivyo wanajua tabia na mienendo yao katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku. Wabunge wengi wamekuwa wakilalamikiwa kukiuka maadili kwa kuwa shughuli za Bunge zinaonekana moja kwa moja kupitia runinga, hivyo kuonekana kuwa wanaongoza katika kukiuka maadili lakini sio kweli, Ofisi imeshughulikia malalamiko mengi kutoka kwa wananchi dhidi ya viongozi mabali mbali na si wabunge na walikuwa na tuhuma nzito kuliko hata mabishano yanayotokea Bungeni.

 

 1. SWALI: Je mwananchi atakuwa na usalama kiasi gani iwapo atamtaja fulani kuwa amekiuka maadili?

 

JIBU: Ofisi ya Maadili ina watumishi ambao wanazingatia maadili yao ya kazi kwa kuweza kutunza siri za ofisi. Sheria pia imeipa mamlaka Ofisi ya Maadili kushughulikia malalamiko ambayo hayana jina la mlalamikaji, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi juu ya uvujaji wa taarifa zao. Kuna baadhi ya malalamiko ambayo ni lazima jina la mlalamikaji lijulikane, mfano ikitokea mwajiriwa anamlalamikia mwajiri wake kwa kumnyanyasa au kutomlipa haki zake hapo lazima jina la mlalamikaji lijulikane ili mwajiri atambue ni nani anayelalamika ili aweze kupata haki yake. Usiri wa taarifa za wananchi upo kwa kiwango cha juu sana isipokuwa inategemea na aina ya lalamiko linalotufikia ofisini.

 

 1. SWALI: Je Ofisi inatoa motisha yoyote kwa wananchi ili watoe taarifa za viongozi wanaokiuka maadili?

 

JIBU: Suala la maadili ni suala la tabia na linahitaji litoke ndani mwa mtu. Mtu mwenyewe atambue ubaya wa jambo analoliona na awe tayari kulitolea taarifa bila hata kupewa motisha wa fedha. Watu wote wawe tayari kutoa taarifa bila hata kupewa motisha wowote wakitambua kuwa kila mmoja analo jukumu la kulinda taifa letu.

 

 

 1. SWALI: Je, ni maadili gani viongozi wanatakiwa kuzingatia?

JIBU: Kifungu cha 6 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kimeorodhesha mambo ambayo kiongozi anatakiwa kuzingatia, pamoja na mambo mengine, kiongozi wa umma anatakiwa afanye kazi kwa uaminifu,huruma ,kujizuia na tamaa na kuzingatia viwango vya juu vya maadili ili imani ya wananchi na matumaini katika uadilifu, haki na kutopendelea kwa serikali vilindwe na kuimarishwa.

 

 1. SWALI: Je, ni mali na madeni yapi ambayo kiongozi anatakiwa atolee tamko?

JIBU: Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

 

 

 1. SWALI: Je, kama kiongozi akiwekeza mali zake kwa mtoto wake inakuwaje?

 

JIBU: Sheria imetaja pia mali za watoto wa kiongozi husika zinatakiwa pia kutolewa tamko na endapo kiongozi ataficha hizo mali basi sheria itachukua mkondo wake.

 

 1. SWALI: Je, kiongozi ambaye hajatoa Tamko la Mali na Madeni atachukuliwa hatua gani?

JIBU: Kutojaza Fomu za Tamko la Mali na Madeni ni kosa kisheria na pia ni ukiukaji wa maadili. Sheria imeainisha adhabu katika kifungu cha 8(a-g) cha Sheria ya Maadili kuwa ni kiongozi kuonywa na kupewa tahadhari, kushushwa cheo, kusimamishwa kazi, kufukuzwa kazi, kumshauri kiongozi ajiuzuru wadhifa unaohusu ukiukaji huo, kupewa adhabu nyingine zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria za nidhamu kuhusu wadhifa wa kiongozi na kuhimiza kuchukuliwa hatua kwa kiongozi kwa mujibu wa sheria za nchi zilizopo. Lakini zipo sababu za kibinadamu zilizo za msingi zinaruhusiwa kutolewa na kiongozi husika ili kujitetea kwa nini alichelewa kutoa tamko na iwapo sababu sio za msingi ndipo sheria huchua mkondo wake kwa huyo kiongozi hupewa adhabu kulingana na uzito wa kosa.

 

 1. SWALI: Hivi ni kweli mwenye pesa ndio mwenye haki na mnyonge hana haki. Msemo huo una ukweli kiasi gani?

 

JIBU: Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

 

 1. SWALI: Je, mwananchi wa kawaida anaruhusiwa kuona Tamko la Mali na Madeni la kiongozi yeyote?

 

JIBU: Mwananchi wa kawaida ana haki ya kuona Daftari la Mali na Madeni ya viongozi ila kwa masharti matatu, kwanza ni lazima mwananchi huyo awe ana lalamiko dhidi ya kiongozi husika, pili mhe. Kamishna wa Maadili anatakiwa kijiridhisha kutokana na lalamiko lililomfikia mezani baada ya kuridhika mwananchi huyo atalipa kiasi cha shilingi 1,000/= kwa ajili ya kuona daftari hilo. Baada ya kuangalia mali za kiongozi husika mwananchi huyo haruhusiwi kutumia taarifa hizo kwa matumizi binafsi, inabaki kuwa  ni siri yake na ofisi tu.

 

 1. SWALI: Je, kiongozi aliyeondolewa madarakani baada ya kukiuka maadili anaweza kuchukuliwa hatua nyingine ya kisheria?

JIBU: Kiongozi aliyekiuka maadili anaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria nyingine kama ilivyofafanuliwa katika kifungu cha 29 cha Sheria ya Maadili kuwa matumizi ya sheria nyingine yanaruhusiwa ikiwemo Sheria ya Kuzuia Rushwa na sheria au kanuni nyingine.

 

 1. SWALI: Wananchi wanaweza kusaidia vipi katika utekelezaji wa Sheria ya Maadili?

JIBU: Wananchi wana nafasi kubwa ya kusaidia kutekeleza Sheria ya Maadili kwa kufichua maovu mbali mbali ya viongozi na kuwasilisha malalamiko yao katika Ofisi za Maadili. Ofisi itayashughulikia malalamiko hayo kwa kuyafanyia uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria. Wananchi wanatakiwa kuchagua viongozi walio na maadili ili watende kazi zao kwa uadilifu kwani wananchi ndio wanafahamu watu waadilifu na hivyo wachague viongozi waadilifu ili watende haki.