ETHICS TRIBUNAL

  BARAZA LA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

 1.0 Utangulizi

          Baraza la Maadili linaundwa kwa mujibu wa fungu la 22(5) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 (Sura 398) kufanya uchunguzi wa kina wa malalamiko ya ukiukwaji wa maadili baada ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kukamilisha uchunguzi wa awali   na kubaini kwamba kuna hoja za kutosha ambapo kiongozi wa umma anapaswa kutoa maelezo bayana ya matendo yake au mali zake. Kuundwa kwa Baraza kunakidhi matakwa ya misingi ya haki na usawa  yanayoainishwa chini ya  Ibara ya 13(6)(a)  ya Katiba ambayo inazitaka mamlaka za nchi kuweka taratibu  zinazozingatia misingi  kwamba wakati haki na wajibu wa mtu yeyote inapohitajika kufanyiwa uamuzi na Mahakama ama chombo kingine chochote kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa  kwa ukamilifu na haki ya kukata rufani ama kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na uamuzi wa Mahakama au chombo kinginecho kinachohusika

1.1 Muundo wa Baraza la Maadili

 Kwa mujibu wa fungu la 26 la Sheria ya Maadili, Baraza la Maadili linatakiwa kuwa na wajumbe watatu wanaoteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, miongoni mwao akiwemo aliyeteuliwa kutoka miongoni mwa wadhifa au amewahi kuwa na wadhifa wa Jaji wa Mahakama ya Rufaa au Jaji wa Mahakama Kuu,  wengine wawili watateuliwa kwa ushauri wa Kamishna wa Maadili. Wajumbe wa sasa wa Baraza waliapishwa Mwezi Mei,  mwaka 2010 kama ifuatavyo,  Mwenyekiti wa Baraza ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa  (Mst.), Mhe. Damian Zefrin Lubuva ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wajumbe wawili, Mhe. Balozi Jaji (Mst.) Hamisi Amiri Msumi na Katibu Mkuu (Mst.) Bw.  Gaudios Tibakweitira.

 1. Kazi za   Baraza  la Maadili
 • Kufanya uchunguzi wa wazi na wa kina wa malalamiko ya ukiukwaji wa maadili.
 • Kufanya uchunguzi wa  tuhuma nyingine zozote dhidi ya kiongozi husika au kiongozi mwingine wa umma kwa agizo la Kamishna wa Maadili
 •  Kuwasilisha taarifa ya uchunguzi wake kwa Kamishna wa Maadili katika kipindi kisichozidi siku 45 tangu kuteuliwa kwake.
 • Kutoa mapendekezo kuhusu hatua za kiutawala, mashtaka ya jinai au hatua nyingine zozote za kuchukuliwa kwa kadri litakavyoona inafaa.
 1. Uwezo wa kisheria (legal powers)

Ili kufanikisha utendaji wake wa kazi, Baraza la Maadili limepewa uwezo wa kisheria kama ifuatavyo:-

 • Kutoa amri ya wito (Summons) kwa mtu yeyote ambaye kwa maoni ya Baraza ataweza kutoa habari yoyote inayohusu jambo lolote kuhusiana na uchunguzi unaoendeshwa na Baraza.
 • Kumtaka yeyote atoe taarifa, hati, kumbukumbu, maandishi au vitu anavyoweza kuwa navyo au kuwa chini ya udhibiti wake.
 •   Kumtaka mtu yeyote kuhudhuria mbele ya Baraza la Maadili katika muda na mahali palipoidhinishwa.
 • Uwezo wa kumuhoji mtu yeyote.
 • Kutoa kiapo na kuamuru mtu yeyote atoe ushahidi chini ya kiapo.
 • Uwezo wa kimahakama wa kuweka kima au kukataa kiasi chochote cha ada ama posho au matumizi mengine.
 •  Kuhoji mwenendo, hati, kumbukumbu, maandishi au vitu vilivyoko chini ya ulinzi wa mamlaka ya Serikali katika Wizara, Idara au Chama cha Siasa au Shirika la Umma.
 • Kutoa amri ya kukamatwa mtu yeyote kuletwa mbele ya Baraza.
 • Uwezo wa kutumia huduma za ushauri wa kitaalam au watu wengine kwa uendeshaji bora wa mwenendo wa uchunguzi.
 • Uwezo wa kuomba msaada kutoka vyombo vingine vya uchunguzi likiwemo Jeshi la Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
 • Uwezo wa kuwazuia baadhi ya Wandishi wa Habari au wote likiona kuwa ipo haja ya kufanya hivyo kwa ajili ya kulinda na kudumisha amani au uendeshaji bora wa Baraza.

1.4 Utekelezaji wa majukumu ya Baraza la Maadili

Baraza la Maadili linatekeleza majukumu yake kwa njia ya vikao. Aina ya kwanza ya vikao vya Baraza ni vikao vya utekelezaji kwa ajili ya kujadili na kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu yake. Vikao hivi huitishwa mara nne kwa mwaka kwa maana nyingine kila baada ya miezi mitatu. Aidha, vikao vya dharura vinaweza kuitishwa kwa wakati wowote linapojitokeza suala ambalo haliwezi kusubiri vikao vya kawaida.

 Aina ya pili ya  vikao, ni vikao vya Baraza  kusikiliza malalamiko ya ukiukwaji wa maadili dhidi ya viongozi wa umma yanayowasilishwa mbele yake na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi. Idadi ya vikao vya kusikiliza malalamiko hutegemea uwepo wa malalamiko yanayostahili kuchunguzwa kwa kipindi husika. Mpaka sasa Baraza limekaa kwa awamu mbili (Mwezi April na June 2011) na  kusikiliza jumla ya malalamiko 40. Maoni na mapendekezo ya Baraza yaliwasilishwa kwa Mhe. Rais  na hatua zilichukuliwa kwa mujibu wa Sheria.

1.5 Mwenendo wa mashauri yanayoendeshwa na baraza

Kwa mujibu wa fungu la 26(5) la Sheria ya Maadili, Baraza la Maadili linatakiwa kufanya uchunguzi wake hadharani isipokuwa kama litaagizwa vinginevyo. Aidha, kwa uendeshaji bora wa mwenendo wa uchunguzi Baraza la Maadili linaweza:-

 •  Kuamuru mtu yeyote atoe ushahidi kwa kiapo na mjumbe yeyote akasimamia kiapo hicho.
 •  Kuomba ushauri wa kitaalamu kadri litakavyoona inafaa
 •  Kuomba msaada kutoka vyombo vingine vya uchunguzi.
 1. Taarifa ya uchunguzi wa baraza
 • Taarifa ya uchunguzi inatakiwa kuwasilishwa kwa Kamishna wa Maadili ndani ya   siku 45 tangu kuteuliwa kwake.
 • Nakala ya taarifa hiyo itawasilishwa kwa Rais, Spika na Mamlaka ya Nidhamu ya kiongozi na kwa kiongozi wa umma husika.
 • Nakala ya Taarifa hiyo inapaswa kuwasilishwa Bungeni na Spika katika kipindi kisichozidi siku saba (7) baada ya kikao cha Bunge kitakachofuata baada ya kupokea taarifa hiyo.
 • Katika taarifa yake, Baraza linaweza kutoa mapendekezo kuhusu hatua za kiutawala, jinai au hatua nyingine zozote zinazostahili kuchukuliwa dhidi ya kiongozi husika. 
 •  Endapo Baraza litaona tuhuma zimetolewa kwa nia mbaya, mzaha, chuki au maelezo hayatoshelezi kuendelea kufanya uchunguzi litabainish hivyo katika taarifa yake.
 1. Taratibu za kuwasilisha wito wa kuhudhuria mbele ya  Baraza la Maadili.
 • Kwa mujibu wa fungu la 24 (1)  Baraza linaweza  kutoa amri ya wito (Summons) kwa  mtu yeyote  kuhudhuria katika Baraza ambaye kwa maoni ya Baraza, ataweza kutoa habari yoyote  kuhusu  jambo lolote linalochunguzwa na Baraza na kumtaka mtu huyo kutoa hati, kumbukumbu , maandishi  au vitu anavyoweza kuwa navyo  au kuwa chini ya udhibiti wake.
 • Amri hiyo itawasilishwa kwa mtu aliyeandikiwa na mtu mwenye wadhifa katika Baraza au Afisa wa Polisi kwa utaratibu uliowekwa wa kuitwa shaurini kwa shahidi katika shauri la madai (civil case) mbele ya mahakama.

1.6.1 Amri ya kukamatwa

 • Amri hii inatolewa iwapo mtu aliyekabidhiwa wito wa kuhudhuria katika Baraza hatafika kwa wakati na mahali palipotajwa kwenye wito na baada ya kuridhika kwamba amri ya wito ilitolewa na iliwasilishwa ipasavyo, ama mtu aliyepelekewa anakwepa kwa makusudi kupokea wito, Baraza linaweza kutoa amri ya kukamatwa mtu huyo na kuletwa mbele ya Baraza. Kila amri ya kukamatwa inayotolewa itatekelezwa na Afisa wa Polisi.
 1. Haki za mashahidi

Kwa mujibu wa Fungu la 24(6) la Sheria ya Maadili mtu yeyote anayetakiwa kuhudhuria ana haki ya kulipwa ada, posho na matumizi kama anavyolipwa shahidi wa Mahakama. Vilevile kila mtu anayetakiwa kutoa taarifa au kuhudhuria ili kutoa ushahidi au kutoa nyaraka zozote,  kumbukumbu,  maandishi  au kitu chochote mbele ya Baraza  atakuwa na haki na hisani(rights and privilege) sawa  kama wanavyopewa mashahidi katika Mahakama Kuu kuhusu nyaraka, kumbukumbu na vitu vingine (Fungu 2 la Sheria)

 


Ibara ya 13(6) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977