Client Service charter

Dibaji:

Mkataba wa Huduma kwa Mteja ulianza kutumika mwaka 2005 kwa mara ya kwanza kwa madhumuni ya kuainisha makubaliano kati ya watoa huduma Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na wapokea huduma ambao ni wananchi wote. Makubaliano hayo yanahusu haki zao (wapokea huduma), wajibu wetu, (watoa huduma), haki za watumishi na namna ya kuwasilisha maoni kulingana na ubora wa huduma zilizotolewa. 

Mkataba wa awali ulikidhi matakwa ya kipindi hicho, lakini kutokana na changamoto kadhaa kama mabadiliko ya kiuchumi, kiteknolojia, kisiasa, kijamii hususani mtazamo na uelewa wa wananchi katika kudai huduma bora, kumekuwa na hisia kwamba huduma tunazozitoa hazikidhi matarajio ya wateja wetu.  Katika kipindi cha miaka minne (4) cha utekelezaji yapo masuala ambayo yametupa fursa ya kujitambua na kufahamu kwa kina ni maeneo gani yanahitaji maboresho.

Ili mkataba huu uwe nyenzo muhimu kwetu katika kusimamia viwango vya huduma na kuongeza uwajibikaji wetu, ni lazima tubainishe mambo yote muhimu ya kuzingatiwa na pande zote mbili.

Mkataba huu una lengo la kuweka bayana huduma zetu, viwango vya utoaji huduma, kusisitiza umuhimu wa wateja wetu kutoa maoni, ushauri na hata kulalamika wasiporidhika na viwango vya huduma tuzitoazo. Hii itasaidia kuufanya mkataba huu kuwa endelevu na kiungo kati yetu na wateja wetu.

Tunawakaribisha wateja wetu wa ndani na wa nje ili watumie fursa ya kuhudumiwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieiti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.  

KAMISHNA WA MAADILI

     Novemba, 2010

1.0  CHIMBUKO LA SEKRETARIETI YA MAADILI

 • Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilianzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na ilianza kazi rasmi mwezi wa Julai mwaka 1996.

 

 • Sekretarieti ilianzishwa ili kutekeleza Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria Na. 13 ya mwaka 1995 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 5 ya mwaka 2001.

 1.1     MUUNDO WA SEKRETARIETI

 1. Sekretarieti ya Maadili ni Idara ya Serikali inayojitegemea chini ya Ofisi ya Rais.

 

 1. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaongozwa na Kamishna wa Maadili ambaye ni  Mtendaji Mkuu.

 

 1. Chini ya Kamishna wa Maadili kuna Makatibu wawili;  mmoja anashughulikia  Watumishi Viongozi wa Utumishi wa Umma na mwingine Viongozi wa Siasa.

 

 1. Kuna Baraza la Maadili lenye mamlaka ya kuchunguza na kusikiliza malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma.

 

 1. Kuna Ofisi sita za Kanda kama zinavyoonekana ukurasa 12 na 13.

1.2.      DIRA YETU

Ni kuwa kitovu cha ubora na ufanisi katika kukuza na kusimamia misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

1.3       DHIMA YETU

Kutoa mwongozo wa kukuza, kusimamia na kudhibiti viwango vya tabia na mwenendo wa kimaadili ili kuhakikisha uzingatiaji wa masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 pamoja na kuwashirikisha Wadau wote katika kufikia lengo hilo.

2.0      MAADILI YETU YA MSINGI

 Katika kutoa huduma kwa wateja wetu tumedhamiria kufuata maadili yafuatayao:-

 • Kutoa huduma kulingana na mahitaji ya Mteja
 • Kutopendelea katika kutoa huduma
 • Kufanya kazi kwa kuzingatia matokeo
 • Kuwa na juhudi kazini na ubunifu.
 • Kuheshimu Sheria, Wajibu, Majukumu, Taratibu na haki  za Wateja wetu
 • Kuwajibika kwa wote
 • Kuwa na matumizi mazuri ya fedha na taarifa
 • Kulinda mahusiano mazuri na wateja
 • Kutoa huduma kwa Uadilifu,Uwazi na Uaminifu
 • Kufanya kazi kwa ushirikiano

3.0       MAJUKUMU YETU

 1. Kupokea na kuhakiki taarifa za Mali na Madeni zinazopaswa kutolewa na Viongozi  wa Umma.
 2. Kupokea malalamiko na tuhuma kutoka kwa wananchi kuhusu Viongozi wanao kiuka maadili.
 3. Kufanya uchunguzi wa awali kuhusu tuhuma au malalamiko dhidi ya kiongozi yeyote wa umma anayetuhumiwa kukiuka maadili.
 4. Kuwaelimisha viongozi wa Umma na Wananchi kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na majukumu ya Sekretarieti.
 5. Kutunza daftari la Mali na Madeni ya Viongozi wa Umma.
 6. Kuwasilisha kwa Rais mapendekezo ya Baraza la Maadili kuhusu uchunguzi wa tuhuma za viongozi wanaokiuka maadili.
 7. Kusimamia na kuendesha Mfuko wa Uadilifu, Uwajibikaji na Uwazi.

4.0       MADHUMUNI

Madhumuni ya Mkataba huu ni kukuza uelewa wa Wateja wetu juu ya aina na viwango vya huduma tuzitoazo ili kumwezesha Mteja kujua atarajie nini na endapo huduma zitatolewa chini ya kiwango kilichoahidiwa, afahamu taratibu za kufuata ili kutoa maoni yake kwa nia ya kupata huduma kulingana na matarijio yake.

5.0       WATEJA WETU

Wateja wetu ni:-

 • Wananchi
 • Viongozi wa Umma
 • Bunge
 • Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali na Serikali za Mitaa
 • Asasi za Kiraia
 • Washirika wa Maendeleo
 • Vyombo vya habari
 • Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

6.0  HAKI ZA WATEJA WETU

            Haki za Viongozi wa Umma

 • Kupata Fomu za Tamko kuhusu Rasilimali na Madeni katika muda muafaka.
 • Kuheshimiwa, kupewa faragha na kutunziwa siri  
 • Kutoa malalamiko
 • Kupewa taarifa zinazomhusu kulingana na Sheria na taratibu zilizowekwa

Haki za Wananchi

 • Kuwasilisha malalamiko dhidi ya ukiukwaji wa Maadili ya Viongozi wa Umma
 • Kujulishwa kuhusu hatua na matokeo ya malalamiko  yaliyowasilishwa
 • Kuheshimiwa, kupewa faragha na kutunziwa siri 
 • Kukagua Daftari la Rasilimali na Madeni kwa kuzingatia taratibu na Sheria zilizopo
 • Kuelimishwa kuhusu maadili na majukumu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. 

              Haki za Bunge

 • Kupata taarifa ya utekelezaji wa majukumu yetu
 • Kujali mapendekezo ya makadirio ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kila mwaka.
 • Kuhoji matumizi ya fedha na rasilimali zilizotolewa.

            Haki za Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali na Serikali za Mitaa:-

 • Kuwasilisha malalamiko dhidi ya ukiukwaji wa maadili ya Viongozi wa Umma
 • Kujulishwa kuhusu hatua na matokeo ya malalamiko waliyowasilisha.
 • Kutunziwa siri na kupewa faragha.
 • Kupelekewa malalamiko yaliyo chini ya mamlaka yao.
 • Kupata ushirikiano katika masuala ya maadili.

           Haki za Asasi za Kiraia

 • Kuwasilisha malalamiko dhidi ya ukiukwaji wa Maadili ya Viongozi wa Umma
 • Kujulishwa kuhusu hatua na matokeo ya malalamiko  yaliyowasilishwa
 • Kuheshimiwa, kupewa faragha na kutunziwa siri 
 • Kukagua Daftari la Rasilimali na Madeni kwa kuzingatia taratibu na Sheria zilizopo
 • Kuelimishwa juu ya majukumu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma
 • Kujengewa uwezo na kushirikishwa katika kukuza Maadili na kuimarisha Utawala Bora

           Haki za Washirika wa Maendeleo

 • Kupata taarifa na kuhoji matumizi ya fedha na  Rasilimali nyingine

            Haki za Vyombo vya Habari

 • Kupata taarifa kulingana na Sheria na taratibu zilizopo
 • Kuelimishwa kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma
 • Kujengewa uwezo na kushiriki katika kukuza Maadili na kuimarisha Utawala Bora

         Haki za Watumishi wetu

 • Kupata fursa za kujiendeleza Kitaaluma
 • Kulipwa stahili zao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa.
 • Kuthaminiwa katika utendaji wao wa kazi.
 • Kusikilizwa na kupewa fursa ya kutoa maoni au ushauri.
 • Kushiriki katika Vikao na Mikutano inayowahusu.
 • Kupewa taarifa za matukio mbalimbali.
 • Kupewa taarifa kuhusu matokeo ya tathmini ya utendaji wao.
 • Kutunziwa siri, kuheshimiwa na kupewa faragha.

7.0       WAJIBU WA WATEJA

Ili kutuwezesha kukupa huduma kwa ubora unaoutarajia, una wajibu ufuatao:-

 • Kufuata sheria, miongozo na taratibu za kuwasilisha malalamiko yako.
 • Kutoa taarifa sahihi kuhusu malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya Viongozi wa Umma
 • Kuwaheshimu watumishi wetu.
 • Kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni kwa mujibu wa Sheria
 • Kutoa ushirikiano kila itakapohitajika
 • Kutunza siri na kuwa muadilifu

8.0       WAJIBU WETU

 • Kuweka viwango vya huduma na kuhakikisha vinafuatwa
 • Kuwa wawazi, kutoa taarifa sahihi na kwa wakati
 • Kupata ushauri na kuwashirikisha wadau muhimu katika masuala ya maadili
 • Kuhakikisha huduma zinawafikia walengwa
 • Kutoa huduma bila upendeleo
 • Kujifunza na kuboresha huduma
 • Kuwa wabunifu ili kutoa huduma bora zaidi
 • Kutunza siri na kuwaheshimu wateja wetu
 • Kuzingatia masuala mtambuka na anuai za jamii

9.0 AINA NA VIWANGO VYA HUDUMA TUNAZOTOA

9.1  IDARA YA VIONGOZI WA UMMA NA WA SIASA

Idara hizi zinasimamia Viongozi wa Siasa na Viongozi wa Utumishi wa Umma ili kuhakikisha masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yanazingatiwa ipasavyo.  Ahadi na Viwango vya huduma tunazotoa:-

 1. Tutatuma Fomu za Tamko la Mali na Madeni kwa Viongozi wa Umma ndani ya miezi 3 kabla ya tarehe iliyowekwa kwa Viongozi wa Umma kuwasilisha Tamko la Mali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili.
 2. Tutakiri kupokea Tamko la Rasilimali na Madeni kutoka kwa Viongozi wa Umma ndani ya siku 14 za kazi baada ya Tamko kupokelewa.
 3. Tutafanya uchambuzi wa malalamiko na kutoa ushauri ipasavyo kuhusu tuhuma za ukiukaji wa Sheria ya Maadili ndani ya siku 14 za kazi baada ya kupokea malalamiko.
 4. Tutafanya uchunguzi wa awali kuhusu tuhuma au malalamiko dhidi ya kiongozi yeyote wa Umma, na kuandika taarifa ya uchunguzi huo ndani ya miezi 6 tangu lalamiko kupokelewa.
 5. Tutakiri kupokea barua za malalamiko na kutoa taarifa za hatua zilizochukuliwa ndani ya siku 14 za kazi baada ya malalamiko kupokelewa.
 6. Tutajibu barua za maombi ya kukagua Daftari la Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma ndani ya siku 21 za kazi baada ya maombi kupokelewa.
 7. Tutafanya tathimini ya utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika maeneo yanayolalamikiwa na wateja.
 8. Tutatoa elimu kwa wadau wetu kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kila itakapohitajika.
 9. Tutatoa taarifa za tafiti mbalimbali tulizofanya kuhusu hali ya Maadili ya Viongozi wa Umma kila itakapohitajika.

9.2       IDARA YA UTAWALA NA UTUMISHI

Majukumu ya Idara hii ni kutoa huduma za Utawala na usimamizi wa Rasilimali Watu katika Sekretarieti ya Maadili. Ahadi na Viwango vya huduma tunazotoa:-

 1. Tutawasilisha majalada kwa watendaji ndani ya dakika kumi na tano (15) tangu ombi kupokelewa masjala;
 2. Tutafanya marekebisho ya mishahara baada ya mabadiliko ya mishahara ya watumishi ndani ya siku 14 za kazi baada ya vielelezo vyote kukamilika na vikao husika kutoa maamuzi.
 3. Tutatoa barua za ajira mpya baada ya vikao vya Kamati Maalum ya Ajira ndani ya siku 14 za kazi baada ya mwajiri kutoa idhini ya kuajiri.
 4. Tutajibu barua/madokezo ya watumishi wanaohitaji ufafanuzi/ruhusa ndani ya siku 3 za kazi baada ya kupokea barua/dokezo.
 5. Tutatoa barua za kupandishwa vyeo kwa watumishi ndani ya siku 3 za kazi baada ya kuidhinishwa na Kamishna wa Maadili.
 6. Tutatoa kibali cha maombi ya likizo ndani ya siku 3 za kazi baada ya kupokea maombi yaliyokamilika na endapo mtumishi anastahili.
 7. Tutashughulikia maombi ya mafao kwa watumishi wastaafu na kuyawasilisha kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii husika ndani ya siku 7 za kazi baada ya kupokea maombi yaliyokamilika.
 8. Tutajibu malalamiko mbalimbali ya watumishi ndani ya siku 3 za kazi baada ya kuyapokea.
 9. Tutaandaa na kusambaza kwa Wajumbe mihutasari ya vikao mbalimbali ndani ya siku saba (7) baada ya vikao.
 10. Tutaandaa na kusambaza Fomu za OPRAS kwa watumishi wote ifikapo tarehe 15 Juni ya kila mwaka.
 11. Tutawezesha malipo ya watoa huduma kufanyika ndani ya siku 3 za kazi baada ya kupokea Ankara za madai.

9.3    KITENGO CHA HABARI ELIMU NA MAWASILIANO

Kitengo hiki kina jukumu la kutoa elimu kwa umma na kuratibu mawasiliano kati ya wananchi na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Ahadi na Viwango vya huduma tunazotoa:-

 1. Tutajibu maswali yamsingi ya Waandishi wa Habari na wadau wengine kwa muda muafaka mara baada ya kuyapokea na kwa yale yanayohitaji ufafanuzi zaidi yatapata majibu ndani ya siku tano (5) za kazi.
 2. Tutatoa machapisho na nyaraka mbali mbali zinapohitajika ndani ya dakika 30 kwa wateja wanaokuja Ofisini kwetu.
 3. Tutatoa Elimu kwa Umma ili kukuza uelewa kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kila inapohitajika.

9.4       KITENGO CHA UNUNUZI NA UGAVI

Kitengo hiki kinatoa huduma kwa wateja katika masuala yahusuyo ununuzi na ugavi wa vifaa, ushauri, ujenzi na huduma. Ahadi na Viwango vya huduma tunazotoa:-

 1. Tutawezesha upatikanaji wa vifaa vinavyohitajika ndani ya siku 5.
 2. Tutajibu maombi yanayopokelewa ndani ya siku tatu (3) za kazi.
 3. Tutaandaa na kutangaza Mpango wa Ununuzi wa mwaka ifikapo tarehe 30 Juni ili kufanikisha shughuli za Ofisi.
 4.  Tutatoa ushauri kuhusu shughuli zinazohusu Ununuzi na Ugavi mara inapohitajika.
 5. Tutaandaa na kutangaza Nyaraka za Zabuni kwa njia mbalimbali:
 • Zabuni za kitaifa (National Competitive Bidding) ndani ya siku 30.
 •  Zabuni za Kimataifa (International Competitive Bidding) ndani ya siku 45.
 1. Tutapokea na kujibu maombi ya Wazabuni kwa muda wa siku 30 kwa Wazabuni wa kitaifa, na siku 45 kwa Wazabuni wa Kimataifa.
 2. Tutaandaa  na kutoa Mikataba kwa Wazabuni ndani ya siku 7 baada ya Zabuni kuidhinishwa
 3. Tutatoa taarifa kwa Mamlaka ya Ununuzi na Ugavi na Wazabuni kuhusu matokeo ya Zabuni ndani ya siku 7 baada ya idhini kutolewa.

9.5       KITENGO CHA UHASIBU

Kitengo hiki kinahusika na upokeaji, utunzaji na kufanya malipo ya fedha ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Sekretarieti.

Ahadi na Viwango vya huduma tunazotoa:-

 1. Tutalipa madai ya fedha yaliyoidhinishwa ndani ya siku 3 za kazi bada ya kupokea maombi ya malipo husika.
 2. Tutaoa taarifa za Fedha za kila mwezi ifikapo tarehe 7 ya mwezi unaofuata.
 3. Tutatoa taarifa Suluhishi za Hesabu za mwezi kila ifikapo tarehe 7 ya mwezi unaofuata mwezi wa taarifa.
 4. Tutatoa taarifa za Robo mwaka kila ifikapo tarehe 21 ya Mwezi Oktoba, Januari na Aprili.
 5. Tutajibu hoja za ukaguzi ndani ya siku 21 baada ya kupokea hoja.
 6. Tutatoa taarifa ya hesabu ya mwaka kila ifikapo tarehe 30 Septemba.

9.6       KITENGO CHA UKAGUZI WA NDANI

Kazi zakitengo hiki ni kuhakikisha kwamba sheria na taratibu za matumizi bora ya rasilimali za umma, manunuzi na taratibu za kiutawala zinafuatwa na kuzingatiwa.

Ahadi na Viwango vya huduma tunazotoa:-

 1. Tutatoa taarifa na ratiba ya ukagauzi unaotarajiwa kufanyika kabla ya siku 7.
 2. Tutatoa taarifa ya majumuisho (Exit Conference/Meetings) kuhusu ukaguzi   kila mwisho wa robo mwaka.
 3. Tutatoa taarifa ya Ukaguzi ya robo mwaka ndani ya siku 10 za kazi baada ya ukaguzi.

9.7    KITENGO CHA TEKNOLOJIA YA HABARI NA MAWASILIANO (ICT)

Kitengo hiki kina wajibu wa kusimamia, kuratibu na kushauri juu ya matumizi ya TEKNOHAMA ndani ya Sekretarieti. Ahadi na Viwango vya huduma tunazotoa:

 1. Tutashughulikia maombi ya matengenezo ya vifaa na mifumo ya teknohama kama ifuatavyo:-
 • Kutafiti na kutatua tatizo ndani ya  masaa 6 baada ya kupokea maombi.
 • Tutatatua tatizo kubwa ndani ya siku 3 baada ya kupokea maombi.
 1. Tutaweka programu mbalimbali za kompyuta ndani ya saa 3 baada ya kupokea maombi.
 2. Tutabuni Mifumo mbalimbali ya kurahisisha utendaji kazi kwa kutumia TEKNOHAMA ndani ya miezi 3 baada ya kupokea maombi.
 3. Tutatoa ushauri kuhusu upatikanaji wa vifaa vya TEKNOHOMA ndani ya siku 3 baada ya kupokea maombi.
 4. Tutaweka taarifa ya matukio mbalimbali ya Taasisi kwenye mtandao kila siku.
 5. Tutatoa taarifa kuhusu matumizi na maendeleo ya teknohama inayohitajika kila baada ya miezi 3.
 6. Tutatoa mafunzo ya matumizi ya teknohama kila itakapohitajika.

9.8    KITENGO CHA MIPANGO

Kitengo hiki kina majukumu ya kuandaa mipango na bajeti, kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mipango ya Sekretarieti na kuandaa taarifa za utekelezaji.

Ahadi na Viwango vya huduma tunazotoa:

 1. Tutatoa taarifa za utekelezaji kutokana na Mpango Mkakati wa Sekretarieti.
 2. Tutatoa rasimu za hotuba ya bajeti ya kila mwaka.
 3. Tutawezesha upatikanaji wa Mpango Mkakati na bajeti ya utekelezaji kila  itakapohitajika.
 4. Tutawezesha upatikanaji wa mwongozo wa uandaaji wa bajeti kila ifikapo Mwezi Novemba.

9.9   MFUKO WA UADILIFU, UWAJIBIKAJI NA UWAZI (FEAT)

Mfuko huu unalenga kuimarisha na kuzijengea uwezo Idara za Serikali (OWIs), Taasisi za Kitaaluma (PAs) na Asasi za Kiraia (CSOs) zinazojishughulisha na uimarishaji wa Utawala Bora hapa Tanzania kwa kuwapa rasilimali.

Ahadi na Viwango vya huduma tunazotoa:

 1. Tutatoa taarifa kuhusu shughuli na madhumuni ya Mfuko kwa Umma na Wadau kila itakapohitajika.
 2. Tutatoa matangazo ya kukaribisha maombi ya kupata Ruzuku kutoka kwa Taasisi, Asasi na Mashirika, pamoja na Wadau wa Mfuko kila baada ya miezi sita (6).
 3. Tutatoa Fomu za maombi ya Ruzuku kwa Wadau ndani ya miezi miwili (2)  baada ya tangazo  kutoka.
 4. Tutapokea maombi ya Ruzuku na kutoa mrejesho ndani ya siku saba (7) baada ya maombi kupokelewa.
 1. Tutatoa taarifa ya uchambuzi wa awali wa maombi ya Ruzuku kwa Kamati ya Uendeshaji wa Mfuko ndani ya miezi mitatu baada ya tarehe ya mwisho ya kupokea maombi ya Ruzuku.
 2. Tutatoa taarifa ya uidhinishwaji wa maombi ya Ruzuku kwa Wadau waliokidhi vigezo ndani ya siku saba (7).
 3. Tutasaini na Wadau Mikataba ya fedha za ruzuku ndani ya siku Thelathini (30) baada ya kuidhinishiwa ruzuku.
 4. Tutatuma Fedha za Ruzuku kwa Wadau walioidhinishiwa maombi yao ndani ya siku tano (5) baada ya kusaini Mikataba ya fedha.
 5. Tutatoa taarifa ya ufuatiliaji na tathmini wa Miradi inayopata ruzuku kutoka katika Mfuko kila robo mwaka (ndani ya miezi mitatu).
 6. Tutatoa taarifa ya robo mwaka ya matumizi ya fedha za Mfuko ndani ya siku kumi na tano (15) baada ya tarehe ya mwisho  ya kila robo  mwaka.
 7. Tutatoa taarifa ya Utendaji na ya fedha ya shughuli za Mfuko kila baada ya miezi sita (6).
 8. Tutatoa elimu kwa umma kuhusu majukumu ya Mfuko wa Uadilifu, Uwajibikaji na Uwazi kila itakapohitajika.

10.0  KUFUATILIA, KUPOKEA MAONI NA KUTOA TAARIFA

10.1    Kufuatilia na Kupokea Maoni

Tunaamini kuwa, usimamizi na ufuatiliaji wa mara kwa mara na utoaji wa taarifa kuhusu viwango vya huduma tunazotoa itatusaidia kufikia viwango vya juu katika kutoa huduma kwa wateja wetu.  Hivyo basi tunaahidi kupima utendaji wetu kwa kufanya yafuatayo:-

 • Tutatoa nafasi kwa wateja wetu ili waweze kutoa mrejesho na maoni kuhusu ubora wa huduma wanazopata kutoka kwetu kwa kutumia njia mbalimbali kama vile Sanduku la Maoni katika Ofisi zetu, barua, simu, barua pepe, kuwasiliana ana kwa ana, nukushi, n.k.
 • Kufanya utafiti na kuanzisha njia sahihi za kufanya ufuatiliaji wa utoaji huduma kwa wateja na wadau.

10.2    Kutoa Taarifa

Tutawajibika kutoa taarifa kuhusu utoaji wa huduma kulingana na ubora wa viwango vilivyoainishwa kwenye Mkataba wa Huduma kwa Mteja.  Hivyo tumekusudia kuimarisha mahusiano na wateja wetu na kutumia mrejesho kutoka kwao ili kuboresha huduma tunazotoa.

11.0   MASUALA YA JUMLA

  KUPOKEA SIMU

Tutapokea simu ndani ya miito mitatu kwa siku za kazi kuanzia saa 1.30 asubuhi hadi saa 9.30 alasiri.

 KUJIBU BARUA

Tutakiri mapokezi ya barua ndani ya siku 7 za kazi tangu barua kupokelewa.

 KUPOKEA WAGENI

Wageni watapokelewa mapokezi na kuelekezwa kunakohusika ndani ya dakika 5 kwa siku za kazI.

DHARURA

Dharura zitashughulikiwa haraka iwezekanavyo kila zinapojitokeza.

MAVAZI

Tutalinda na kuheshimu Maadili ya Mtanzania katika Mavazi yaliyokubalika na jamii kama ilivyofafanuliwa katika Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 3 wa mwaka 2007 unaohusu Mavazi

LUGHA

Lugha itakayotumika kutoa huduma ni Kiswahili au Kiingereza kulingana na tukio au mahitaji ya mteja.

 TUNU

Tutathamini na kulinda usalama wa watumishi na wateja wetu kwa kuzuia vitendo vyote vinavyohatarisha usalama katika maeneo ya kazi.

MAHUSIANO

Tutajenga na kuimarisha mahusiano mema kwa wateja wa ndani na wa nje ili kuleta ufanisi.

SAA ZETU ZA KAZI

Ofisi zetu zitakuwa wazi kuanzia saa 1.30 asubuhi hadi saa 9.30 alasiri kwa siku za kazi kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa.

 MIADI

Miadi kuhusu kupata majibu na kuwa na mikutano itazingatiwa kulingana na taratibu zilizowekwa.

 MAPITIO YA MKATABA

Ili Mkataba wetu uwe endelevu tunaahidi kuupitia kila baada ya miaka 6 kwa kuwashirikisha wadau na wateja wetu.

12.0    MAWASILIANO YETU

Tunakaribisha maoni, ushauri, malalamiko kuhusu ubora wa utoaji wa huduma zetu kwa njia zifuatazo:-

Tuandikie kupitia anuani:-

1.    KAMISHNA WA MAADILI

Ofisi ya Rais,

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,

S.L.P. 13341,

DAR ES SALAAM.

 • Tupigie kwa Simu Na. +255 22 2111810/11, +255 22 2136422
 • Tuandikie kwa Nukushi Na.  +255 22 2119217, +255 22 2137269
 • Tutumie barua pepe – secretariat@ethics.go.tz
 • Ofisi yetu ipo Plot No. 109/32 na 110/32 Mtaa wa Ohio mkabala na Ofisi za Ubalozi wa Zambia.