Kamishna Nsekela awahimiza viongozi kujaza Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa usahihi


Kamishna Nsekela awahimiza viongozi kujaza Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa usahihi
21
Aug
2017

Kamishna Nsekela awahimiza viongozi kujaza Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa usahihi.

Kamishna wa Maadili Jaji (Mst.) Harlod Nsekela amewataka viongozi wa umma kutoa taarifa za usahihi wakati wanapojaza fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni.

Kamishna Nsekela aliyasema hayo Agosti 21, 2017 wakati akiwaapisha kiapo cha uadilifu maafisa kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi. Hafla ya kiapo hicho imefanyika katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma jijini Dar es Salaam.

Mhe. Nsekela alifafanua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995, kiongozi wa umma anatakiwa kujaza fomu ya Tamko la Rasilimali na Madeni siku 30 baada ya kushika madaraka na kila ifikapo Desemba 31 kila mwaka.

Jaji Nsekela alisema, “Fomu za tamko la Rasilimali na Madeni zinapaswa kujazwa kwa usahihi wa hali ya juu na kuziwakilisha katika ofisi za Sekretarieti ya Maadili.”

Kwa mujibu wa Sheria ya Maadili, baada ya fomu hizo kuwasilishwa, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma hufanya uhakiki wa awali kwa kuangalia usahihi wa ujazwaji wake ili kubaini kama matakwa ya kisheria yamezingatiwa.

Aidha Kamishna alisema kuwa kulingana na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka1995kifungucha18 (3) (a) kinaipa Sekretarieti mamlaka ya kumuita kiongozi yeyote na kumhoji kuhusiana na tuhuma za ukiukwaji wa Sheria ya Maadili.

Pia Kamishna aliongeza kuwasheriaya Maadili ya Viongozi wa Umma kifungu cha 18 (2) (d) na (e) kinaipa Sekretarieti ya Maadili mamlaka ya kufanya uhakiki wa mali za kiongozi kulingana na tamko lake la Raslimali na Madeni na kufanya uchunguzi. Aidha, uhakiki huo unazihusu pia rasilimali na madeni ya mwenza wa kiongozi pamoja na watoto wake walio chini ya umri wa miaka 18.

Kamishna Nsekela aliwataka maofisa hao wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi kutoa ushirikiano kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakati wa zoezi la uhakiki pindi litakapofanyika.

“Toeni ushirikiano kwetu na mzingatie uadilifu katika utendaji wenu wa kazi ili kuendana na kasi ya awamu ya tano,” amesema.

Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma hufanyika mara moja katika utumishi wa Kiongozi wa Umma tofauti na ujazaji wa Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni ya viongozi wa Umma ambapo kiongozi wa umma hutakiwa kujaza ifikapo Desemba 31, ya kila mwaka.