Maswali Yaulizwayo Mara kwa MaraKila mwananchi anatakiwa kuifahamu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Kwa kuifahamu Sheria hiyo wataisaidia Ofisi kwa kutoa taarifa za ukiukwaji wa maadili unaofanywa na viongozi mbali mbali. Wananchi wanaweza kupata elimu ya maadili kupitia njia mbali mbali kama vile redio, semina na matukio ya kitaifa ambayo yanakusanya watu wengi kwa pamoja kwa mfano maadhimisho ya sherehe za wakulima nchini(nanenane) ambapo Ofisi ya Maadili huwa inatoa elimu kwa umma katika banda la maadili. Elimu inatolewa pia kupitia kipindi cha redio na kipindi maalum cha maadili kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) siku ya Jumatatu na Star tv siku ya Jumanne kuanzia saa moja kamili hadi saa moja na nusu jioni. Hivyo, wananchi wanashauriwa wafuatilie ili kujifunza zaidi majukumu ya ofisi yetu.

Ofisi ya Maadili haifanyi kazi kama kisiwa. Inashirikiana na ofisi nyingine kama vile ofisi ya RPC, RPO, Mkuu wa Mkoa na ofisi nyingine katika kutekeleza majukumu mbali mbali. Kwa kuwa rushwa ni moja ya vitendo vya ukiukaji wa maadili, Ofisi ya Maadili hushirikiana na TAKUKURU kwa ajili ya kukamata viongozi wanaojihusuisha na rushwa

Suala la maadili ni suala la tabia na linahitaji litoke ndani mwa mtu. Mtu mwenyewe atambue ubaya wa jambo analoliona na awe tayari kulitolea taarifa bila hata kupewa motisha wa fedha. Watu wote wawe tayari kutoa taarifa bila hata kupewa motisha wowote wakitambua kuwa kila mmoja analo jukumu la kulinda taifa letu.

Uvunjifu wa maadili kwa kiasi kikubwa unatokana na viongozi kuwa na mgongano wa maslahi yaani kutanguliza maslahi binafsi badala ya kutanguliza maslahi ya umma. Pindi, wananchi wanapokumbana na viongozi wa aina hiyo wasisite kufika katika Ofisi za Maadili kutoa taarifa kuhusu viongozi wa aina hiyo. Hakuna kiongozi ambaye yuko juu ya sheria. Mtendaji Kata au Kijiji analipwa mshahara ambao unatokana na kodi za wananchi hapaswi kumtoza pesa kwa ajili ya kupewa huduma. Wananchi nao waondokane na dhana kuwa huwezi kupewa huduma hadi utoe rushwa.

Kila mwananchi anapaswa kuijua Sheria ya Maadili si lazima awe kiongozi. Kwa viongozi wa umma Ofisi ya Maadili huwa inatoa mafunzo kwa viongozi wanapochaguliwa au kuteuliwa ili kuwaeleza misingi ya maadili na mipaka ya utendaji kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

Ofisi ya Maadili ina watumishi ambao wanazingatia maadili yao ya kazi kwa kuweza kutunza siri za ofisi. Sheria pia imeipa mamlaka Ofisi ya Maadili kushughulikia malalamiko ambayo hayana jina la mlalamikaji, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi juu ya uvujaji wa taarifa zao. Kuna baadhi ya malalamiko ambayo ni lazima jina la mlalamikaji lijulikane, mfano ikitokea mwajiriwa anamlalamikia mwajiri wake kwa kumnyanyasa au kutomlipa haki zake hapo lazima jina la mlalamikaji lijulikane ili mwajiri atambue ni nani anayelalamika ili aweze kupata haki yake. Usiri wa taarifa za wananchi upo kwa kiwango cha juu sana isipokuwa inategemea na aina ya lalamiko linalotufikia ofisini.

Wananchi wanatakiwa kupeleka malalamiko yao katika ofisi za maadili zilizopo Tabora mjini, mtaa wa Jamhuri, jengo la NSSF, ghorofa ya pili. Hapo mwananchi atasikilizwa lalamiko lake bila kutozwa gharama yoyote ile na hatua zitachukuliwa. Aidha, mlalamikaji halazimiki kutaja jina lake na taarifa zake huwa ni siri kati ya mwananchi na Ofisi ya Maadili. Malalamiko yanaweza kuwasilishwa kwa njia ya simu, barua, ana kwa ana. Baada ya kupokelewa malalamiko hayo hufanyiwa uchuguzi na ikibainika kama kweli kuna ukiukwaji wa maadili, kiongozi husika hushtakiwa kwenye Baraza la Maadili na kuhojiwa kutokana na tuhuma za ukiukaji wa maadili zinazomkabili, kisha Baraza hutoa mapendekezo na mapendekezo hayo hupelekwa kwa Rais kwa hatua zaidi. Kwa viongozi ambao hawaguswi na Sheria ya Maadili, kwa mfano watendaji wa kata na vijiji wao wanawajibika kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa na Wilaya husika. Sheria inamuwajibisha Mkurugenzi ili awawajibishe watendaji wake wa chini kama mtendaji wa kijiji kata na mtaa.

Orodha ya viongozi wa umma imeainishwa katika kifungu 4(1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Aidha, Mhe. Rais ameongeza orodha ya viongozi mwaka 2013.

JIBU: Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilitungwa mwaka 1995 ili kudhibiti tabia na mienendo ya viongozi wa umma. Hii ni kufuatia kukosekana kwa kwa chombo/sheria ya kusimamia maadili ya viongozi wa umma tangu mwaka 1992 baada ya kufutwa kwa Sheria ya Kamati ya Kusimamia utekelezaji wa Miiko ya Viongozi ya mwaka 1973 kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa. Viongozi wakawa hawazingatii tena uadilifu hivyo likatolewa pendekezo la kutungwa kwa sheria ambayo itasimamia maadili ya viongozi wa umma.