Jaji Mipawa ateuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili.


Jaji Mipawa ateuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili.
16
Aug
2019

Jaji Mipawa ateuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli hivi karibuni amemteua Jaji Mstaafu Ibrahim Sayida Mipawa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.

Jaji Mipawa anachukua nafasi ya Jaji Mstaafu Januari Msofe ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria.

Kwa mujibu wa Fungu la 26(1) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 pamoja na marekebisho yake linaeleza kuwa Baraza litakuwa na watu watatu watakaoteuliwa na Rais, miongoni mwao akiwemo aliyeteuliwa kutoka miongoni mwa watu wenye wadhifa au wamewahi kuwa na wadhifa wa Jaji wa Mahakama Kuu. Aidha, Fungu hilo hilo la 26 kifungu kidogo cha (3) kinasema kuwa Rais, atateua mmojawapo wa Wajumbe wa Baraza kuwa Mwenyekiti.

Kazi kubwa ya Baraza la Maadili ni kufanya Uchunguzi wa Kina wa malalamiko yanayohusu ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya viongozi wa umma waliotajwa katika Fungu la 4 la Sheria hiyo. Aidha, uchunguzi huo hufuatiwa na uchunguzi wa awali ambao kwa mujibu wa Fungu la 18 (2)(c) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma hufanywa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Jaji Ibrahim Sayida Mipawa anakuwa Mwenyekiti wa nne wa Baraza la Maadili akitanguliwa na Jaji (Mst.) Damian Lubuva, Jaji (Mst.) Hamis Msumi na Jaji (Mst) Januari Msofe.