Jaji Mkuu amlilia Kamishna wa Maadili


Jaji Mkuu amlilia Kamishna wa Maadili
15
Dec
2020

Jaji Mkuu amlilia Kamishna wa Maadili

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma, hivi karibuni aliwaongoza waombolezaji kuuzika mwili wa Marehemu Mhe. Jaji (Mst.) Harold Reginald Nsekela jijini Mbeya.

Marehemu Jaji (Mst) Nsekela aliyefariki dunia tarehe 6 Desemba, 2020 jijini Dodoma, alikuwa Kamishna wa Maadili katika Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Mhe. Jaji Mkuu wakati wa mazishi hayo aliwaeleza waombolezaji kuwa maisha ya marehemu Jaji Nsekela yalilenga kuwabadili watu wengine tangu alipokuwa mhadhiri katika chuo kikuu cha Afrika Mashariki mwaka 1968.

“Mhadhiri wa chuo kikuu anafundisha sheria ili kuwabadili watu na kuwa na watumishi wazuri. Alifanya kazi ambayo inabadilisha watu wengine,” alisema na kuongeza kuwa “alipokuwa akifanya kazi katika Shirika la Sheria Tanzania alikuwa anatoa huduma ambayo ilikuwa inawabadilisha watu wengine na muda wake mwingi aliutumia kazini, lakini matunda ya kazi yake ni makubwa sana.”

Kwa mujibu wa Jaji Ibrahimu, Marehemu Nsekela alikuwa na sifa mbalimbali wakati wa utumishi wake ikiwemo kuaminiwa na Marais watatu katika vipindi tofauti tangu mwaka 1997 alipotuliwa na Rais Benjamin William Mkapa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

“Marehemu alikuwa na sifa ya kuaminiwa na Marais. Sio kazi nyepesi kwa mtu yoyote kuaminiwa na Rais, kuna watu zaidi ya milioni 55 hapa nchini, lakini unakuta wewe ndio unaaminiwa katika kazi fulani. Sasa Jaji Nsekela aliaminiwa na Rais Benjamin William Mkapa, Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, wote walimuamini huyu mtu.”

Ni watu wachache sana wanapata bahati ya kuaminiwa na Rais mmoja sembuse unaaminiwa na Marais watatu.

Aidha Jaji Mkuu aliongeza kuwa sifa nyingine ya Marehemu Jaji Nsekela ni kuaminiwa sana na majaji Wakuu mara alipoteuliwa kuwa Jaji.

“Nakumbuka tarehe 10 Desemba, 1998 aliteuliwa na Jaji Mkuu Francis Nyalali kuwa mmoja wa majaji watatu walioanzisha divisheni ya Mahakama ya Biashara wakati huo Tanzania ilikuwa inatoka katika siasa za mashirika ya umma na kuingia katika sekta binafsi na Mahakama ya Biashara ilikuwa ni jambo muhimu sana.”

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu Prof. Ibrahim, Marehemu Nsekela aliaminiwa sana na Jaji Mkuu Barnabas Samata kuwa Mwenyekiti wa bodi ya watu waliotengeneza “Law reforms.” Jaji Nsekela alisimamia bodi hiyo iliyotengeneza hukumu zilizokuja kutumiwa na watu wengine kufanya kazi za kisheria.

“Hii ni imani kubwa sana ambayo alipewa,” alisema na kuongeza kuwa Jaji Mkuu Samata alimteua pia kuwa mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Majaji.

“Wengi huwa wanadhani ukiwa kiongozi unakuwa juu ya sheria, hata sisi tunawajibika kufuata sheria, tunawajibika kufuata taratibu kama raia wengine wote. Jaji ambaye alikuwa akikiuka utaratibu, huwa tunakamati ambayo inakaa, inafanya uchunguzi na kutoa mapendekezo katika Tume ya Mahakama kuhusu mwenendo wa jaji husika na huyo Jaji anaweza kuondolewa kazini, kwa hiyo, kazi ya maadili aliianzia Mahakamani.

Mhe. Prof. Ibrahimu Jumaa aliitaja sifa nyingine ya Marehemu Jaji Nsekela kuwa ni mtumishi aliyeg’ang’aniwa katika utumishi wa umma.

Alisema, “alipofikisha miaka 65 hakukubaliwa kustaafu. Na hiyo ni sifa, kuna wengine wanaomba kustaafu unaambiwa sawa haraka haraka, lakini huyu alikuwa anaomba anakataliwa.”

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema katika Ibara ya 120 (3) iwapo Rais ataona kuwa kwa ajili ya manufaa ya umma, Jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani ametimiza umri wa miaka 65 huwa anakataa asisitaafu.

Ibara ya 120 (3) inasema, iwapo Rais ataona kuwa kwa ajili ya manufaa ya umma inafaa Jaji wa Mahakama ya Rufani aliyetimiza umri wa miaka sitini na tano aendelee kufanya kazi, na Jaji huyo wa Rufani anakubali kwa maandishi kuendelea kufanya kazi, basi Rais aweza kuagiza kuwa Jaji huyo wa Rufani aendelee kufanya kazi kwa muda wowote utakaotajwa na Rais.”

Jaji Nsekela alipofikisha umri wa miaka 65 tarehe 21 Oktoba, 2009 hakukubaliwa kustaafu, Rais wa Awamu ya Nne alimuongezea miaka miwili. Akasema sasa utastaafu tarehe 21 oktoba, 2011. Tarehe hizi zilipokaribia taarifa zikaja nyingine kuwa hakuna kustaafu tena. Akaongezewa mwaka mmoja na kuambiwa utastaafu tarehe 21, Oktoba, 2012. Kabla ya tarehe hiyo kufika, ikajitokeza sifa nyingine kwasababu majaji wa Afrika Mashariki wanapendekezwa na Marais wa nchi zote zile wakae waangalie sifa zako kama unafaa.

“Hata alipomaliza muda wake, bado umma ulikuwa unamuhitaji. Hakukaa kulea wajukuu wate, aliteuliwa kuwa Kamhsina wa Maadili katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Desemba, 2016.”

Wakati huo huo, Jaji Mkuu alieleza kuwa Jaji Nsekela alikuwa akisaidia sana Mahakama pale ambapo viongozi mbalimbali walipokuwa wakivunja sheria, Katiba au kuingilia uhuru wa Mahakama.

“Tulikuwa tunashitaki kwa Jaji Nsekela na wengi waliitwa na kuhojiwa ingawa tulikuwa tunafanya kazi kimya kimya. Kwa hiyo alikuwa na msaada mkubwa sana kama mkiona viongozi wa umma wanakiuka sheria mpelekeni Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ataitwa na kuojiwa kwa usiri na hatua zitachukuliwa.

Viongozi wengine walioudhuria maziko hayo ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. Albert Chalamila, Jaji Kiongozi Dkt Eliezar Feleshi na viongozi wengine wa chama na Serikali.