Kamishna Mwagesi awakumbusha Watumishi wa Sekretarieti kutunza siri za Serikali.


Kamishna Mwagesi awakumbusha Watumishi wa Sekretarieti kutunza siri za Serikali.
23
Aug
2021

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi amewataka watumishi wa Sekretarieti ya Maadili kutunza siri za serikali pamoja na kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Hayo ameyasema wakati akizindua Baraza jipya la Wafanyakazi la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma lililofanyika katika ukumbi wa VETA, mkoani Iringa tarehe 20 Agosti, 2021.

“Kikatiba Taasisi yetu ndiyo inayotegemewa kwenye masuala yanayohusiana na Maadili. Hivyo ni vema tutambue kuwa tumepewa dhamana ya kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake na sisi ndiyo taswira ya Taifa letu linapokuja suala la uadilifu, hivyo tuwe waadilifu na wasiri kuonesha mfano kwa wengine”. Alifafanua Mhe Mwangesi

Mhe. Mwangesi aliendelea kusisitiza kuwa ili watumishi wa Sekretarieti ya Maadili wasikose kuaminiwa mbele ya jamii na Serikali, kupitia kikao hicho aliwaomba kila mmoja ajitafakari kwa kina kama kwa matendo na mwenendo wake anafaa kuwa miongoni mwa watumishi wa Taasisi hiyo na kisha aone namna ya kujirekebisha ili waweze kwenda pamoja, kuhifadhi jina na hadhi ya Taasisi na kuongeza imani yao kwa wadau wao na jamii kwa jumla.

Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazoathiri utendaji wao wa kazi ambazo ni pamoja ufinyu wa bajeti, upungufu wa vitendea kazi na upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali, Mhe. Mwangesi alisema kuwa wanaendelea kupambana kwa lengo la kukabiliana na changamoto hizo kwa kuchukua hatua mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mhe. Mwangesi, hatua hizo ni pamoja na kuishawishi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa iweze kuwasemea Bungeni hasa katika Kamati ya Bajeti kuweza kuwapatia nyongeza ya fedha za uendeshaji wa Taasisi ili kupata utatuzi wa changamoto nyingine zinazotegemea uwepo wa fedha.

Hatua nyingine zinazochukuliwa ili kukabiliana na changamoto hizo ni kuiomba Wizara ya Fedha na Mipango kuiongezea Taasisi ukomo wa bajeti (sealing) pamoja na kupata vibali vya kujaza nafasi za watumishi zilizowazi kwa utaratibu wa ajira mpya ama kuhamishiwa watumishi kutoka Taasisi nyingine.

Kuhusu ushirikiano, Mhe. Mwangesi alitumia msemo wa kiafrika unaosema kuwa “ukitaka kwenda kwa haraka nenda peke yako, na ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako” akikazia umuhimu wa ushikiano katika kazi.

“Mimi kama kiongozi wenu nimechagua kwenda mbali.Hivyo basi, sualala ushirikiano baina yetu halina mbadala na ninachoshauri kwa kila mmoja wetu ni ushiriki wa dhati kwani hii Sekretarieti ya Maadili ni yetu sote na kufanikiwa kwake ndiyo kufanikiwa kwetu”Alibainisha Mhe. Mwangesi.

Mhe. Mwangesi aliendelea kusema kuwa kila mtumishi kwa nafasi yake na ushiriki wake, tutekeleze majukumu yetu kwa weledi, maarifa, jitihada na mapenzi; kuanzia mpokea barua hadi Kamishna wa Maadili, kwani lengo letu ni moja tu la kujenga nyumba tuliyokabidhiwa na tusiikwamishe Serikali kutekeleza majukumu yake kiujumla na yeyote atakayekwamisha utekelezaji wa majukumu tuliyokabidhiwa hatavumiliwa kamwe.

Mkutano huo wa Siku moja wa Baraza la Wafanyakazi la Sekretarieti ya Maadili ni utekelezaji wa Waraka wa Rais Namba 1 wa mwaka 1970 ambao unaelekeza kila Taasisi ya Umma kuwa na Baraza la Wafanyakazi ili kuimarisha Dhana ya Utatu baina ya Serikali, Mwajiri na Wafanyakazi ili kuleta ufanisi mahala pa kazi.