Mhe Nsekela: Hakuna muda wa nyongeza kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma baada ya Desemba 31.


Mhe Nsekela:  Hakuna muda wa nyongeza kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma baada ya Desemba 31.
30
Dec
2019

Viongozi wa Umma wanaowajibika na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma wameelezwa kuwa hakutokuwa na muda wa nyongeza kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma baada ya Desemba, 31 mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela wakati akitoa tathmini ya hali ya urejeshaji wa matamko ya rasilimali na madeni ya viongozi wa umma kwa Waandishi wa Habari jijini Dodoma hivi karibuni.

Mhe Nsekela alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma haina mamlaka ya kisheria ya kuongeza muda na kwamba chombo chenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tumekuwa tukiwakumbusha viongozi wa umma mara kwa mara kurejesha matamko yao Sekretarieti ya Maadili lakini mpaka sasa hali ya urejeshaji hairidhishi” alibainisha Mhe. Nsekela.

Akizungumzia hatua zitakazochukuliwa dhidi ya viongozi ambao hawatowasilisha matamko yao baada ya Desemba 31, Mhe. Nsekela alisema kuwa kushindwa kuwasilisha tamko la rasilimali na madeni katika muda uliowekwa na Sheria ni kosa chini ya fungu la 15 (a) na kwamba Sekretarieti ya Maadili haitosita kuchukua hatua za kisheria dhidi yao ikiwemo kuwafikisha katika Baraza la Maadili.

“Si makusudio yetu na sio nia yetu kuwafikisha watu kwenye Baraza la Maadili kwa jambo dogo la kushindwa kutoa tamko, ila ikibidi tutafanya hivyo.Yale ambayo yatawatokea viongozi ambao watakuwa hawajawasilisha matamko yao ndani ya muda uliowekwa na sheria wasije kumlauma mtu” alifafanua Mhe. Nsekela.

Kuhusu kutoa tamko la uongo, Mhe. Nsekela alisema kuwa kutoa tamko la uongo ni kosa chini ya fugu la 27 (2) kosa ambalo ukitiwa hatiani adhabu yake ni kutozwa faini si chini ya shilingi milioni moja na si zaidi ya shilingi milioni tano au kifungo kisichozidi mwaka mmoja.

Akitoa tathmini ya hali ya urejeshaji wa matamko ya rasilimali na madeni ya viongozi hadi kufikia tarehe 20 Desemba, 2019 Mhe. Nsekela alikiri kuwa sio nzuri.

Kwa mujibu wa Mhe. Nsekela hadi kufikia tarehe 20 Desemba, 2019 kati ya viongozi wa umma 13,699 wanaotakiwa kuwasilisha tamko kwa Kamishna wa Maadili ni viongozi 2,369 tu ambao ni sawa na asilimia 17 ndio waliowasilisha matamko yao kwa Kamishna wa Maadili.

Mhe. Nsekela aliendelea kusema kuwa viongozi 11,330 ambao ni sawa na asilimia 83 bado hawajawasilisha matamko yao kwa mujibu wa sheria.

Kutoa tamko la rasilimali na madeni kwa viongozi wa umma ni matakwa ya kikatiba chini ya Ibara ya 132 (5) (b) ambayo inaeleza wazi kuwa moja kati ya misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma itawataka watu wanaoshika nafasi fulani za madaraka kutoa mara kwa mara maelezo rasmi kuhusu mapato, rasilimali na madeni yao pia ni matakwa ya kisheria chini ya fungu la 9 (1) (a)-(c) la Sheria ya Maadii ya viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.