Mhe. Nsekela: Tuna meno ya kusimamia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.


Mhe. Nsekela: Tuna meno ya kusimamia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
09
Jan
2020

Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela amewaambia Waandishi wa Habari kuwa Sekretarieti ya Maadili ina meno katika kusimamia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma nchini.

Hayo ameyasema leo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma alipokuwa akitoa tathmini ya urejeshaji wa Matamko ya Rasilimali na Madeni ya viongozi wa umma mpaka kufikia Desemba, 2019.

Mhe. Nsekela alibainisha kuwa Sekretarieti ya Maadili inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Ibara ya 132 (1) ambayo inayataja Mamlaka ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwa ni kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yanazingatiwa ipasavyo.

Pia, Mhe Nsekela alisema kuwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kupitia Fungu la 8 linaipa meno Sekretarieti ya Maadili kuchukua hatua dhidi ya kiongozi atakayekiuka maadili ambapo alisema kuwa ni pamoja na kuonywa na kupewa tahadhari; kushushwa cheo; kusimamishwa kazi; kufukuzwa kazi na kumshauri kiongozi kujiuzulu wadhifa wake kutokana na ukiukaji huo. Hatua nyingine ni kuhimiza kuchukuliwa hatua kwa kiongozi kwa mujibu wa sheria za nchi zilizopo, alifafanua Mhe Nsekela.

Akitoa tathmini ya urejeshaji wa Matamko mpaka kufika tarehe 31 Desemba, 2019, Mhe. Nsekela alisema kuwa hali ya urejeshaji ni nzuri ambapo alifafanua kuwa Viongozi Wakuu wa Kitaifa wote wakiwemo Mawaziri na Manaibu Waziri wamerejesha matamko yao. Makundi mengine ya Viongozi waliorejesha ni pamoja na Majaji, Makatibu na Manaibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa wote na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Kuhusu hatua iliyofikia ya Mfumo wa Ujazaji wa Tamko kwa njia ya Mtandao Mhe. Nsekela aliwahakikishia Waandishi wa Habari kuwa mfumo umefikia hatua za mwisho na kwamba mwaka huu utaanza kufanya kazi.