Naibu Katibu Mkuu Tamisemi Awataka Maafisa Elimu Kujaza Hati ya Ahadi ya Uadilifu


Naibu Katibu Mkuu Tamisemi Awataka Maafisa Elimu Kujaza Hati ya Ahadi ya Uadilifu
22
Aug
2019

Naibu Katibu Mkuu Tamisemi Awataka Maafisa Elimu Kujaza Hati ya Ahadi ya Uadilifu

Maafisa Elimu Mkoa, Elimu Maalum, Wilaya pamoja na Elimu Watu Wazima Mkoa na Wilaya wametakiwa kujaza Fomu za Hati ya Ahadi ya Uadilifu kwani utekelezaji wa Ahadi hizo utatumika kama kigezo katika uteuzi wa nafasimbalimbali za uongozi.

Agizo hilo limetolewa na Bw. Nzunda mara baada ya uwasilishwaji wa Mada ya Ahadi ya Uadilifu uliofanywa na Kaimu Katibu Msaidizi, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Ofisi ya Kanda ya Kati Dodoma, Bibi Jasmin Awadhi katika Kikao Kazi kilichowakutanisha Maafisa Elimu kutoka kila Mkoa Tanzania Bara kilichofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere uliopo Chuo cha Mipango jijini Dodoma Agosti 21, 2019.

“Ninawaagiza mkajaze Hati ya Ahadi ya Uadilifu kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria.Kwa wale ambao ni Viongozi wa Umma wakishajaza wanatakiwa kumpelekea Kamishna wa Maadili sambamba na Fomu ya Tamko la Mali na Madeni na wale ambao siyo Viongozi wakishajaza wanatakiwa kumpelekea Mkurugezi wa Halmashauri yake” alibainisha Bw. Nzunda.

Bw. Nzunda aliongeza kusema kuwa msingi wa ahadi hizi ulilenga kuwa na Serikali yenye Uwazi, Wajibikaji, Uadilifu na Weledi katika kutekeleza majukumu yake kwa umma.

Aidha, Bw. Nzunda aliwasisitiza Maafisa Elimu hao kuhakikisha kwamba Makampuni wanayofanya nayo kazi yawe yamejaza Hati ya Ahadi ya Uadilifu kwa Sekta Binafsi kwani ushirikishwaji wa Sekta hiyo unalenga kukataa Rushwa na Vitendo vya ukiukwaji wa Maadili

Awali akiwasilisha Mada ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Katibu Msaidizi Idara ya Ukuzaji Maadili, Bw. Salvatory Kilasara aliwasihi Maafisa Elimu hao kuzijua Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995.

“Ndugu Viongozi, Kanuni za Utumishi wa Umma zinatutaka kutii Sheria, sasa tusipozifahamu Sheria itatuletea shidakwa Viongozi wetu pamoja na vyombo vya serikali kama Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma” alisema Bw. Kilasara.

Pia, Bw. Kilasara aliwataka Maafisa Elimu hao kujiepusha na Vitendo vya Mgongano wa Maslahi ambavyo vimekuwa ni tatizo la kimaadili vinavyorudisha nyuma maendeleo ya nchi yetu.

Akitolea mfano wa matumizi ya magari ya serikali, Bw. Kilasara alisema magari hayo siyo ya kubebea nyasi za mifugo au kumpeleka mama saluni, hivyo wayatumie kwa maslahi ya umma na si maslahi binafsi.