Rais Magufuli amuapisha Jaji Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi kuwa Kamishna wa Maadili


Rais Magufuli amuapisha Jaji Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi kuwa Kamishna wa Maadili
24
Dec
2020

Rais Magufuli amuapisha Jaji Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi kuwa Kamishna wa Maadili

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemuapisha Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi kuwa Kamishna wa Maadili, hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino Dodoma.

Mhe. Mwangesi ameshika wadhifa huo baada ya Jaji wa Mahakama ya Rufani Mstaafu Mhe. Harold Nsekela ambaye alikuwa Kamishna wa Maadili kufariki dunia.

Akizungumza baada ya uapisho, Mhe. Dkt. Magufuli aliipongeza Sekretarieti ya Maadili kwa kazi nzuri chini ya uongozi wa aliyekuwa Kamishna wa Maadili Marehemu Harold Nsekela na ana imani kuwa Mhe. Mwangesi ataiendeleza kazi hiyo.

Mhe. Rais alitumia fursa hiyo kuwataka Viongozi wa Umma kutumia muda uliobaki kuwasilisha matamko yao kwani ifikapo Desemba 30 ndio mwisho wa kurejesha matamko hayo kwa mujibu wa Sheria na ndio mana amehakikisha kuwa anamteua Kamishna wa Maadili kabla ya Desemba 30 ili kusiwe na kisingizio kwa viongozi wa umma kushindwa kuwasilisha matamko yao.

Sambamba na hilo, Mhe. Rais ameahidi mbele ya hadhara iliyohudhuria hafla hiyo kwamba yeye mwenyewe atawasilisha tamko lake ndani ya muda uliobaki kabla ya Desemba 30.

Akitoa maoni yake kuhusu Mfumo wa Ujazaji wa Matamko kwa njia ya Mtandao Mhe. Rais alisema kuwa kutumia mfumo huo kutaondoa usiri wa taarifa za viongozi na amewaagiza watendaji wa Sekretarieti ya Maadili kuwaelekeza Viongozi wa Umma kupakua Fomu za Tamko kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Maadili ili wazijaze na kuziwasilisha wao wenyewe katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili kama ambavyo ilikuwa ikifanyika huko nyuma.

Awali akizungumza baada ya kuapishwa, Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Sikalalilwa Mwangesi amemshukuru Mhe. Rais kwa kumuamini kumteua kushika wadhifa huo na ameahidi kuzingatia Sheria, Sera na Ilani ya Uchaguzi katika kusimamia Maadili ya Viongozi nchini kwani Maadili ndio Msingi wa Maendeleo.

Mhe. Jaji Mwangesi anakuwa Kamishna wa Maadili wa tano tangu kuanzishwa kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mwaka 1996.Makamishna wa Maadili waliomtangulia ni pamoja na Mhe. Jaji (Mst.) William John Maina, Marehemu Mhe. Jaji (Mst.) Steven Ernest Ihema, Mhe. Jaji (Mst.) Salome Suzzette Kaganda na Marehemu Mhe. Jaji (Mst.) Harold Reginald Nsekela.