Sekretarieti ya Maadili yajidhatiti kukabiliana na tatizo la Mgongano wa Maslahi miongoni mwa viongozi wa Umma.


Sekretarieti ya Maadili yajidhatiti kukabiliana na tatizo la Mgongano wa Maslahi miongoni mwa viongozi wa Umma.
01
Sep
2020

Sekretarieti ya Maadili imeendelea kujidhatiti vilivyo katika kukabiliana na tatizo la Mgongano wa Maslahi miongoni mwa viongozi wa umma nchini.

Katika kipindi cha miaka mitatu, Sekretarieti ya Maadili imejikita katika kuelezea namna ya kudhibiti masuala ya Mgongano wa Maslahi, kama ilivyofafanuliwa katika fungu la 4 na 5 la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela wakati akifungua kikao kazi cha kujenga uwezo kuhusu Mgongano wa Maslahi kwa baadhi ya Maafisa wa Sekretarieti ya Maadili kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (Mkapa House) jijini Dodoma Septemba Mosi, 2020.

Mhe. Nsekela alibainisha kuwa mwaka 2017 Sekretarieti ya Maadili iliandaa mpango ulioainisha uelekeo wa Taasisi katika kushughulikia masuala yanayohusu Mgongano wa Maslahi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Kwa mujibu wa Mhe. Nsekela, mpango huo umejikita katika Vipengele vikubwa vinne ambavyo ni pamoja na Fichua yaani ‘Disclosure’, Jadili yaani ‘Discuss’, TambuaDetection’ na Kuandaa nyaraka kwa ajili ya ufuatiliaji na tathmini.

“Hadi sasa, vipengele viwili vinavyohusu kufichua na kujadili yameshafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na uwepo wa Sheria ya Maadili ya viongozi wa Umma na Kanuni zake pamoja na uwepo wa baadhi ya nyaraka”.

“Sehemu ya pili inayohusu kipengele cha Jadili yaani ‘Discuss’ ambayo imejikita katika uelewa kuhusu masuala ya Mgongano wa Maslahi kupitia Semina, Warsha na majadiliano baina ya Sekretarieti ya Maadili na Viongozi wa Umma yameanza kushughulikiwa”. Alifafanua Mhe. Nsekela.

Kwa mujibu wa Mhe. Nsekela kipengele cha tatu na cha nne bado havijafanyiwa kazi na kwamba kuna pengo kubwa linalohitaji kushughulikiwa haraka.

Vipengele hivyo ambavyo kimsingi vinahusu ufichuzi yaani ‘detection’ na ufuatiliaji kuhusu udhibiti wa Mgongano wa Maslahi vinahitaji kiasi kikubwa cha maarifa na ujuzi ambao utawezesha kufichua vitendo vya Mgongano wa Maslahi na kufuatilia tabia za viongozi katika eneo hili, alifafanua Mhe. Nsekela.

Katika kukabiliana na hali hiyo Mhe. Nsekela aliainisha maeneo matano ambayo yanatakiwa kujengewa uwezo.Aidha, kwa mujibu wa Mhe. Nsekela maeneo hayo ni pamoja na Ufuatiliaji, Ufichuzi wa vitendo vya Mgongano wa Maslahi, Uwezo wa ndani yaani kuziba pengo la ujuzi na maarifa kuhusu Mgongano wa Maslahi miongoni mwa watumishi wa Sekretarieti.

Maeneo mengine ni Uhamasishaji kwa umma hususani wajibu wao katika kuwafuatilia na kuwatolea taarifa viongozi wanaojihusisha na Mgongano wa Maslahi pamoja na kujenga mifumo mtambuka itakayosaidia katika ufuatiliaji, ufichuzi pamoja na kuishirikisha jamii. Alimaliza kusema Mhe. Nsekela.

Kikao kazi hicho cha siku nne kimewakutanisha baadhi ya Maafisa wa Sekretarieti ya Maadili kutoka Makao Makuu na Kanda nne ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID) kupitia Mradi Endelevu wa Mapambano dhidi ya Rushwa Tanzania (BSAAT).