Sekretarieti ya Maadili yazindua Mfumo mpya wa Ujazaji Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni.


Sekretarieti  ya  Maadili  yazindua  Mfumo  mpya  wa Ujazaji  Fomu za    Tamko la Rasilimali  na Madeni.
07
Apr
2020

Sekretarieti ya Maadili yazindua Mfumo mpya wa Ujazaji Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya Mtandao.

Ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeanza kutumiaMfumo wa Ujazaji wa Matamko ya Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma kwa njia yaMtandao (Online Declaration System - ODS)

Akizindua mfumo huo Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela alisema kuwa mfumo huu umeanzishwa ili kutekeleza Sera ya Serikali Mtandao (e- Goverrment) ambayo Serikali imeagiza Wizara na Taasisi zote za Umma (MDAs) kutumiaMifumo ya TEHAMA katika kurahisisha mawasiliano na utendaji wa kazi Serikalini.

Mhe. Kamishna alieleza kuwa mfumo huu una umuhimu na faida nyingi sana kwani utawawezesha Viongozi kujaza matamko yao kwa urahisi na kwa usahihi zaidi popote pale watakapokua iwe ndani au nje ya nchi.Aidha, Mhe. Nsekela alibainisha kuwa Mfumo utampunguzia kiongozi usumbufu pamoja na kuingia gharama mbalimbali kama vile gharama za kupakua fomu za tamko, kuzijaza na kuzituma kwa njia ya posta ambapo hutumia fedha pamoja na usumbufu wa kutumia muda mrefu kusafiri kutoka katika sehemu alipo kwenda katika ofisi za Sekretarieti kuwasilisha fomu.

Mhe. Nsekela aliendelea kufafanua kuwa mfumo huu utaondoa uwezekano wa kupokea matamko kutoka kwa watumishi ambao sio Viongozi kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa UmmaNa. 13 ya mwaka 1995.

“Toka Sheria hii ilivyotungwa mwaka 1995 tumekuwa na tatizo la kupata takwimu sahihi za Viongozi. Viongozi wengi hawajui kama wao ni viongozi au laa, na wakati mwingine hutoa matamko wakiwa wanakaimu nafasi husika wakati sheria inamtambua kiongozi aliyethibitishwa tu kuwa ndiye kiongozi wa umma hivyo basi mfumo huu utasaidia kupata takwimu sahihi za viongozi” alifafanua Mhe. Nsekela.

Aidha, Mhe. Nsekela alisisitiza kuwa jukumu la viongozi kujaza fomu za tamko la rasilimali na madeni sio ombi bali ni takwa la kisheria na kikatiba. “Napenda kuwakumbusha viongozi wenzangu kuwa hatuombwi kujaza fomu za tamko bali ni takwa la kisheria na tunaamrishwa kufanya hivyo kwani hata kiongozi namba moja katika nchi yetu ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli hutekeleza takwa hilo kila mwaka”alisema Mhe. Nsekela.

Mhe. Nsekela alitumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi wa umma kutoa matamko wakati wa kumaliza kutumikia nyadhifa zao kwani viongozi wengi hawafanyi hivyo na kwa kufanya hivyo wanakiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Naye Katibu Idara ya Ukuzaji Madili, Bw. John Kaole akijibu swali lililoulizwa na mwandishi kuhusu hali ya Maadili nchini ukilinganisha na enzi za Rais wa kwanza wa Zanzibar Hayati Aman Abeid Karume alisema kuwa, Hayati Karume alikua mzalendo na utu na alikua mtu mwenye huruma.

Bw. Kaole aliendelea kufafanua kuwa hapo nyuma baada ya mfumo wa vyama vingi kuanzishwa Maadili kwa Viongozi yaliporomoka ndio maana Sheria ya Maadili ikatungwa ili kudhibiti hali hiyo. Aidha, kuhusu hali ya Maadili katika nchi yetu kwa sasa, Bw. Kaole alisema kuwa kwa sasa hali ni nzuri hususani katika awamu hii ya tano inayoongozwa na Mhe. John Pombe Magufuli kwa kuangalia katika kipengele cha urejeshaji wa matamko ambapo imefikia hadi asilimia 97.

Kwa mujibu wa Bw. Kaole kipengele kingine kinachoonesha hali ya Maadili kuwa nzuri ni kwa kuangalia kuboreka kwa utoaji wa huduma muhimu za kijamii katika sekta mbalimbali kama vile afya, elimu, maji, na nyingine nyingi ambapo Viongozi wengi wanaosimamia maeneo hayo kwa sasa wamekua waadilifu na wazalendo.

Mfumo wa Ujazaji wa Fomu za Tamko kwa njia ya Mtandao unachukua nafasi ya utaratibu wa awali wa kujaza Fomu za Tamko kwa mkono na kuziwasilisha kwa Kamishna wa Maadili ifikapo Desemba 31 ya kila mwaka.Mfumo huu unaanza kufanya kazi rasmi kuanzia leo tarehe 7 Aprili, 2020 ambapo dirisha lipo wazi kwa Viongozi wapya na waliomaliza kutumikia nyadhifa zao baada ya kuwasilisha taarifa zao za siri ikiwa ni pamaja na Majina matatu, namba ya/za simu, barua pepe binafsi, taasisi anayofanyia kazi, Wadhifa/Cheo, tarehe ya uteuzi/kuchaguliwa katika Wadhifa/Cheo husika na kama anakaimu au amethibitishwa katika Wadhifa/Cheo.Aidha, taarifa hizi zinatakiwa kutumwa kupitia anuani ya barua helpdesk@ethicssecretariat.go.tz.