Sekretarieti ya Maadili yazindua Vipindi vya Elimu kwa Umma kuhusu Mgongano wa Maslahi jijini Arusha


Sekretarieti ya Maadili yazindua Vipindi vya Elimu kwa Umma kuhusu Mgongano wa Maslahi jijini Arusha
13
Feb
2020

Sekretarieti ya Maadili yazindua Vipindi vya Elimu kwa Umma kuhusu Mgongano wa Maslahi jijini Arusha

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imezindua vipindi vya elimu kwa umma kuhusu Mgongano wa Maslahi kupitia kituo cha redio cha Sunrise cha jijini Arusha.

Uzinduzi huo ulifanywa na Katibu – Idara ya Ukuzaji wa Maadili katika Sekretarieti ya Maadili Bw. Waziri Kipacha ambaye alisema kuwa lengo la programu hii ni kutoa elimu ya maadili kwa umma na kuimarisha mawasiliano kati ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na wananchi.

“Programu hii ya elimu ya maadili kwa umma kupitia vipindi vya redio inalenga kuimarisha mawasiliano kati ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, viongozi wa umma na wananchi kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995,” alifafanua Bw. Kipacha.

Bw. Kipacha atumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa umma kuzingatia maadili katika utendaji wao wa kazi kwani maadili ya viongozi ni nyenzo muhimu katika kukuza na kuimarisha utawala bora nchini.

“Maaadili ndio msingi wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni,” alisema na kuongeza kuwa, “Uongozi bora unaozingatia maadili mema unapaswa kuwa mfumo wa jamii zetu ili tuweze kufikia maendeleo endelevu.”

Kwa mujibu wa Katibu huyo, Tanzania inahitaji kuwa na safu ya viongozi ambao ni mfano nzuri wa uzingatiaji wa maadili wanaotumia nafasi zao za uongozi kuwaletea wananchi maendeleo.

“Viongozi wana dhima ya kuhakikisha wanazingatia viwango vya juu vya maadili kwa kujiepusha na mgongano wa maslahi ili kuimarisha imani ya wananchi wanapofanya maamuzi,” alibainisha Bw. Kipicha.

Kwa upande wake Katibu Msaidizi Kanda ya Kaskazini Bi. Anna Mbasha alisema kuwa kupitia vipindi hivi, Viongozi wa umma pamoja na wananchi wataelimishwa umuhimu wa maadili kwa mujibu wa Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.

Jumla ya vipindi 52 vya redio vitarushwa kupitia Kituo cha Redio cha Sunrise cha jijini Arusha ikiwa ni utekelezaji wa Mradi wa kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini hususani katika eneo la Mgangano wa Maslahi kwa viongozi wa umma unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza (DFID).

Aidha, idadi ya vipindi kama hivyo vitarushwa katika baadhi ya vituo vya redio katika Kanda ya Magharibi Tabora, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kanda ya Kati – Dodoma, na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini – Mbeya.