Shule ya Msingi Msijute yafanya hafla ya kuwaaga Wahitimu wa Klabu ya Maadili waliohitimu Elimu ya Msingi.


Shule ya Msingi Msijute  yafanya hafla ya kuwaaga Wahitimu wa Klabu ya Maadili waliohitimu  Elimu ya Msingi.
23
Sep
2019

Shule ya Msingi Msijute yafanya hafla ya kuwaaga Wahitimu wa Klabu ya Maadili waliohitimu Elimu ya Msingi.

Wanachama wa Klabu ya Maadili katika Shule ya Msingi Msijute iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mikindani wametakiwa kuwa mabalozi wazuri kwa kuyaendeleza Maadili waliyoyapata shuleni katika kuielimisha jamii baada ya kuhitimu Elimu yao ya Msingi.

Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Katibu Msaidizi, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kusini Mtwara Bw Filotheus Manula katika hafla ya kuwaaga wahitimu hao iliyofanyika katika Ukumbi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kusini Mtwara.

Aidha Bw. Manula katika hotuba yake, alieleza kuwa Maadili ndiyo msingi wa Maendeleo ya nchi na kwa sababu hiyo, tusipokuwa waadilifu, hatutopata maendeleopia Maadili yanatakiwa kuanzia katika Familia hivyo tunatakiwa kuyaendeleza Maadili hayo katika jamii iliyotuzunguka wakiwemo Wazazi.

Bw. Manula pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Mlezi wa Klabu hiyo, Mwalimu Agnes Raphael Chotara, kwa kufanya vizuri katika kuisimamia Klabu hiyo ambayo imekua kivutio kikubwa kwa kuwa na wanafunzi wanaofanya vizuri Kitaaluma pamoja na nidhamu kwa ujumla.

Naye Mwalimu Agnes R. Chotara, ambaye pia ni Mlezi wa Klabu ya Maadili, Shule ya Msingi Msijute, aliipongeza Sekretarieti ya Maadili kwa kuanzisha Vilabu vya Maadili mashuleni ambavyo vimechangia katika kuboresha ufaulu wa wanafunzi wa klabu hiyo pamoja na nidhamu..

Mwalimu Chotara aliongeza kuwa Klabu ya Maadili katika Shule hiyo imeleta matunda mazuri ikiwemo nidhamu miongoni mwa wanafunzi hao. Akithibitisha hilo, alieleza kuwa wanafunzi wanaofanya vizuri kitaaluma, wengi wao ni wale ambao ni Wanachama wa Klabu ya Maadili. Hivyo, aliwasisitiza wahitimu kuendelea kuwa waadilifu hata baada ya kuhitimu elimu ya msingi.

Hata hivyo Wanachama wahitimu wa Klabu hiyo nao hawakuwa nyuma katika kuonesha furaha na hisia zao kwa kupata fursa ya kufika katika Ofisi ya Maadili, ambapo waliipongeza Ofisi ya Kanda kwa ushirikiano inaowapatia katika utekelezaji wa shughuli mbali mbali za Klabu, na kupelekea kuwa na mafanikio makubwa ikiwemo kuwafanya miongoni mwa wanachama kubadilika kitabia mara baada ya kujiunga na Klabu hiyo.

Mmoja wa Wanachama Wahitimu wa Klabu hiyo alieleza kuwa, kutokana na mwitikio mzuri wa wanachama pamoja na usimamizi bora wa Mwalimu Mlezi, katika kipindi cha takriban miaka miwili tangu Klabu hiyo izinduliwe Shuleni kwao, wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanya shughuli mbali mbali ikiwemo kuanzisha mradi wa utengenezaji wa fagio, ambazo huuza na kuwapatia kipato cha kuendeleza shughuli za Klabu hiyo.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwasihi wanachama wenzake wanaoendelea na masomo kuongeza juhudu zaidi katika kuhakikisha kuwa Klabu yao inakuwa na mafanikio makubwa zaidi na hata kuendelea kuwa ya mfano miongoni mwa Vilabu vya Maadili [50] vilivyopo ndani ya Mkoa wa Mtwara, kwa upande wa Shule za Msingi.

Jumla ya Wanachama Wahitimu 24 kutoka Shule ya Msingi Msijute iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, walitunukiwa Vyeti vya Uanachama wa Klabu ya Maadili baada ya kuhitimu Elimu ya Msingi, Septemba 12, 2019.