Viongozi wa Mkoa wa Geita na Simiyu watakiwa kutanguliza maslahi ya Umma mbele kuliko maslahi yao binafsi.


Viongozi wa Mkoa wa Geita na Simiyu  watakiwa kutanguliza maslahi ya Umma mbele kuliko maslahi yao binafsi.
12
Dec
2019

Viongozi wa Mkoa wa Geita na Simiyu watakiwa kutanguliza maslahi ya Umma mbele kuliko maslahi yao binafsi.

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela amewataka Viongozi waliopewa dhamana ya uongozi nchini, kuzingatia matakwa ya Sheria ya Maadili ikiwa ni pamoja na kutanguliza maslahi ya Umma mbele kuliko maslahi yao binafsi.

Mhe. Nsekela aliyasema hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Umma wakati wa ziara aliyoifanya Kanda ya Ziwa katika Mkoa wa Geita pamoja na Kanda ya Magharibi Mkoani Simiyu mapema hivi karibuni kwa lengo la kuwakumbusha Viongozi wa Umma kuhusu uzingatiaji wa matakwa ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya Mwaka 1995.

"Nyinyi viongozi wezangu katika nafasi zenu mlizokabidhiwa msifikirie kuweka mbele maslahi yenu binafsi kwanza, bali maslahi ya umma ndiyo yanapaswa kutangulizwa mbele" alisema Mhe. Nsekela.

Aidha, Mhe. Nsekela amewataka Viongozi wa Umma kutokuwa waongo pindi wanapojaza fomu za Rasilimali na Madeni kwani kwa kufanya hivyo wanakuwa wamekiuka Sheria ya Maadili.

Alisema lengo la Serikali ni kuona Viongozi wake wanakuwa wawazi na waadilifu katika ujazaji wa mali walizonazo na sivyo vinginevyo, hivyo hakuna sababu ya wao kuwa waoga na waongo.

Vilevile Mhe. Nsekela aliwataka Viongozi wa Umma wa Mikoa hiyo kuishi na kuenenda katika kiapo cha Ahadi ya Uadilifu walichoahidi kukifuata pindi wanapoteuliwa kushika nyadhifa zao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Luhumbi akifungua mafunzo hayo ya Maadili alisema, Viongozi na watendaji wamekuwa wakijiingiza kwenye vitendo vya mgongano wa maslahi na hivyo kusababisha kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi.

Alisema kwa mantiki hiyo Viongozi wanahitaji wawe na Maadili ili Tanzania iweze kufikia malengo ya kiuchumi iliyojiwekea na kwa kufanya hivyo imani ya wananchi itaongezeka kwa Viongozi na Serikali yao.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Antony Mtaka mbali na kumshukuru Kamishna wa Maadili kwa ujio wake wa kuja kuongea na Viongozi wa Mkoa huo, pia alitumia fursa hiyo kuomba uwezekano wa kuwasogezea Wananchi na Viongozi wa Mkoa wa Simiyu, Ofisi za Sekretarieti ya Maadili badala ya kufuata huduma hiyo Mkoani Tabora.

“Mheshimiwa Jaji naomba ikikupendeza, Sisi Viongozi na Wananchi wa Mkoa wa Simiyu, Mara na Shinyanga tunaomba tuwe na Kanda yetu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma inayotolewa na Ofisi yako kwani tunalazimika kwenda Tabora ambako ni mbali kutokea hapa” alisema Mhe. Mtaka.