Viongozi wa Mkoa wa Manyara wapewa semina ya Maadili.


Viongozi  wa Mkoa wa Manyara wapewa semina ya Maadili.
01
Jul
2019

Viongozi wa Mkoa wa Manyara wapewa semina ya Maadili.

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Harold Nsekela aliwaasa Viongozi wa Umma wa Mkoa wa Manyara wasiwe kama “ KASUKU” wakati wanapokula kiapo cha Ahadi ya Uadilfu, wakati wanapotekeleza Majukumu yao kama Viongozi .

Kauli hiyo imetolewa na Mhe. Jaji Harold Nsekela katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano kwa Viongozi wa Umma mkoani humo uliohusu Utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na 13 ya mwaka 1995, uliofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara.

Aidha Mhe. Nsekela katika hotuba yake aliwataka Viongozi hao kuheshimu Viapo vyao wanavyoapa kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia Viongozi hao kujenga imani kwa wananchi wanaowaongoza.

Mhe. Nsekela alifafanua kuwa kwa kuheshimu Viapo hivyo pia itawasaidia Viongozi hao kufanya kazi kwa uadilifu, uwazi, usawa ,kutopendelea na pia itawasidia kuepuka mgongano wa Maslahi jambo ambalo ni kinyume cha Maadili kwa Kiongozi yeyote.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Alexander Mnyeti ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika Mkutano huo, aliwataka Viongozi mkoani humo, kufanya kazi kwa Uadilifu na kuepuka mgongano wa Maslahi jambo ambalo ni kinyume cha Maadili ya Viongozi wa Umma.

Mkuu huyo wa Mkoa, alisema kuwa kazi tunazozifanya sisi Viongozi wa Umma, zilenge kuwahudumia wananchi tunaowaoongoza kwa ajili ya Maslahi ya Umma na wala sio kwa Maslahi yetu binafsi

Lengo letu liwe moja la kuwatumikia Wananchi tunaowaongoza kwa kutoa huduma bora na kwa kusimamia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Aliongeza kuwa, kuna baadhi ya Viongozi ambao wanapata fedha kwa njia zisizo halali na kwenda kuzitumia nje ya nchi huko jambo ambalo ni kinyume cha Maadili ya Viongozi wa Umma. Hivyo ni wajibu wa Kiongozi wa Umma kuondokana na tabia hizo ambazo ni Kinyume cha Maadili kama Kiongozi.

Jumla ya Viongozi zaidi ya 60 walishiriki katika Mkutano huo kutoka katika Wilaya mbili Mkoani humo ambazo ni Babati Wilaya pamoja na Babati Mji, ambapo ulihudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Mkoa huo ikiwemo Sekretarieti ya Mkoa wa Manyara, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Taasisisi mbalimbali za Umma, Wakuu wa Idara , pamoja na Waheshimiwa Madiwani.