​Viongozi wa Umma Mkoani Arusha watakiwa kuepuka Mgongano wa Maslahi.


​Viongozi wa Umma Mkoani Arusha watakiwa kuepuka Mgongano wa Maslahi.
01
Jul
2019

Viongozi wa Umma Mkoani Arusha watakiwa kuepuka Mgongano wa Maslahi.

Viongozi wa Umma Mkoani Arusha wametakiwa kufanya kazi zao kwa Uadilifu na kwa kusimamia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika utekelezaji wa Majukumu yao.

Tamko hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo alipokua Mgeni rasmi katika Mkutano uliohusu Maadili kwa Viongozi wa Umma Mkoani humo ambapo alifafanua kwamba, Kazi ya Sektetarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma sio kupambana na Viongozi bali ni kuwasimamia Viongozi hao kufanya kazi zao kwa Uadilifu, Uwazi, Ukweli na bila upendeleo wa aina yoyote ili kujenga na kukuza imani kwa Wananchi wanaowaongoza.

Mkuu huyo wa Mkoa katika hotuba yake alifafanua kuwa, Viongozi wa Umma tunatakiwa kufanya kazi ya kuwahudumia wananchi tunaowaongoza bila kujali itikadi zetu za vyama vya siasa ili kuondoa Mgongano wa Maslahi miongoni mwetu.

Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa majukumu yetu tusiingize maslahi yetu binafsi bali kipaumbele kiwe ni kwa ajili ya maslahi ya Umma , ambapo alisema kuwa kuwepo kwa mgongano wamaslahi ni kiashiria kikubwa cha kuwepo kwa rushwa na maovu mengine ambayo ni kinyume cha Maadili kwa Kiongozi wa Umma.

Mhe. Gambo katika hotuba yake aliongeza kuwa, Unafiki , Majungu na Uongo ni vitu ambavyo havitakiwi katika utendaj i wetu wa kazi tunapokua katika utekelezaji wa majukumu yetu kama Viongozi tunatakiwa kuweka pembeni itikadi za vyama vyetu na kwamba Kiongozi lazima tabia na muenendo wako uendane na sifa yako kama Kiongozi.

Aliwataka Viongozi wa Umma Mkoani humo kujitambua kuwa wao kama Viongozi kila wanachokifanya au wanachoongea katika utekelezaji wa Majukumu yao wanapaswa kufahamu kuwa kuna tafsiri kubwa miongoni mwa wananchi wanaowaongoza. Hivyo ni vyema Viongozi kuwa wavumilivu, kuwa na staha, na pia kufanya kazi kwa kuangalia mazingira husika na kwamba ni ukiukwaji wa Maadili kwa Kiongozi kuzozana na Kiongozi mwenzake mbele ya Wananchi anawaowaongoza.

Aidha Mhe.Gambo aliwaasa Viongozi hao kutovurugwa na siasa katika utekelezaji wa majukumu yao ili kazi wanazozifanya ziangalie Maslahi ya Umma kama Kiongozi na wala sio kwa kuangalia Maslahi binafsi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Viongozi wa Umma kutoka katika Wilaya za Arusha, Arumeru, Ngorongoro, Longido, Monduli na Karatu.