Viongozi wa Umma wahimizwa kutoa Matamko ya kweli ya Rasilimali na Madeni yao.


Viongozi wa Umma wahimizwa kutoa Matamko ya kweli ya Rasilimali na Madeni yao.
06
Dec
2019

Viongozi wa Umma wahimizwa kutoa Matamko ya kweli ya Rasilimali na Madeni yao.

Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela amewataka viongozi wa Umma kutoa taarifa sahihi kuhusu Rasilimali na Madeni yao wakati wa kujaza Fomu ya Tamko ya Rasilimali na Madeni wanayomiliki kama Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inavyotaka.

Kauli hiyo aliitoa leo wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari uliowakutanisha Waziri wa Nchi, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Kapteni (Mst.) George Huruma Mkuchika (Mb) pamoja na Wakuu wa Taasisi zinazojihusisha na Utawala Bora nchini ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu.

Mhe. Nsekela alibainisha kuwa wao kama Sekretarieti ya Maadili wanachohitaji si kurejesha Tamko tu bali umeandika nini ndani ya Tamko hilo. “Je umeandika kweli au sio kweli?Kitu tunachoangalia ndani ya Tamko ni uzingatiwaji wa matakwa ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma” alisisitiza Mhe. Nsekela.

Akilielezea hali ya urejeshaji wa Fomu za Tamko kwa mwaka 2018, Mhe. Nsekela alisema kuwa hali sio mbaya kwani viongozi 15,303 kati ya viongozi 15,592 walirejesha Fomu zao za Tamko ambao ni sawa na asilimia 98.

Kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya Viongozi wanaoshindwa kurejesha Fomu zao au kurejesha nje ya muda uliowekwa kwa mujibu wa Sheria Mhe. Nsekela alisema kuwa kiongozi yeyote asiyerejesha Fomu anakuwa amekiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na anaweza kupelekwa kwenye Baraza la Maadili kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.Kwa mujibu wa Mhe. Nsekela, endapo Baraza hilo litamkuta na hatia hutoa mapendekezo ya adhabukwa kiongozi husika.

Kuhusu suala la nani anayepaswa kurejesha Fomu za Tamko ikiwa kiongozi wa Umma amepata dharura kama vile ugonjwa, Mhe. Nseka alianza kwa kufafanua kuwa Sheria inamtaja kiongozi kwa wadhifa wake na kwamba inatakiwa kiongozi mwenyewe awasilishe Tamko lake kwa sababu ya usalama wa taarifa zake.

Hata hivyo, Mhe. Nsekela alikiri viongozi wakati mwingine hupatwa na dharurana alitolea mfano wa dharura iliyompata Mhe. Freeman Mbowe alivyowekwa mahabusu na kushindwa kuwasilisha Tamko lake kwa wakati lakini Mhe. Mbowe alichukua hatua ya kumwandikia barua Kamishna wa Maadili iliyomtaarifu dharura yake na wao kama Sekretarieti ya Maadili waliipokea na alipotoka mahabusu Mhe. Mbowe aliwasilisha Tamko lake kwa Kamishna wa Maadili kama Sheria inavyomtaka kufanya hivyo.

Awali akisoma taarifa yake kwa Waandishi waHabari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Kapteni (Mst.) George Huruma Mkuchika (Mb.) alisema kuwa wanapoadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu wanatumia fursa hiyo kujitathmini kama nchi namna wanavyozingatia maadili, wanavyodhibiti rushwa katika taifa, wanavyofuata taratibu katika manunuzi ya umma, wanavyowajibika kama Serikali, taasisi na kama mwananchi mmoja mmoja.

Maadhimisho ya mwaka huu wa 2019 yamebebwa na Kauli Mbiu inayosema “ Maadili katika Utumishi wa Umma ni Nguzo Muhimu katika kuimarisha Utawala Bora na Haki za Binadamu.” Kilele cha maadhimisho hayo itakuwa ni tarehe 11 Desemba, 2019 ambapo kutakuwa na Mdahalo utakaowakutanisha Makatibu Wakuu, Manaibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi. Kwa mujibu wa Mhe. Mkuchika, Mdahalo huo utasimamiwa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Mhandisi John Kijazi.