Wajumbe wa Baraza la Maadili wafanya Ziara Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.


Wajumbe wa Baraza la Maadili wafanya Ziara Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
10
Mar
2020

Wajumbe wa Baraza la Maadili wafanya Ziara Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Kamishna wa Maadili Mhe Jaji (Mst.) Harold Nsekela amewatambulisha rasmi Wajumbe wapya wa Baraza la Maadili kwa Menejimenti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mapema mwezi huu.

Wajumbe hao wapya wa Baraza la Maadili waliteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ni pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Ibrahimu Mipawa, Naibu Katibu Mkuu Mstaafu Bibi Immaculate Ngwalle na Katibu Mkuu Mstaafu Bw. Peter Ilomo ambao ni Wajumbe wa Baraza hilo.

Mhe. Jaji Harold Nsekela katika hotuba yake ya utambulisho wa wajumbe hao kwa Menejimenti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma alisema kuwa hili Baraza ni la awamu ya tatu tangu kuundwa kwa Baraza la Maadili ambapo Awamu ya kwanza ya Baraza Mwenyekiti wake alikuwa ni Mhe. Jaji (Mst) Damian Lubuva na wajumbe wake ambao walikuwa ni Mhe. Jaji (Mst) Balozi Msumi na Bw. Gaudius Tibakweitira na Awamu ya pili ya Baraza ilikuwa ni ya Mwenyekiti Mhe. Jaji (Mst) Balozi Hamisi Msumi na Wajumbe wake ni Bibi. Hilda Gondwe na Bibi. Selina Wambura.

Mhe. Nsekela aliendelea kufafanua kuwa Jukumu kuu la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995 ili kuhakikisha kwamba tabia na mienendo ya Viongozi wa Umma waliotajwa katika Fungu la 4(1) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na pia Misingi ya Maadili iliyoainishwa katika Sehemu ya Pili na Sehemu ya Tatu ya Sheria hiyo vinazingatiwa.

“Misingi ya Maadili na Maadili yaliyotajwa katika Sehemu ya Pili na Sehemu ya Tatu ya Sheria, inatoa miongozo ya tabia na misingi ya Maadili inayopaswa kuzingatiwa na Kiongozi wa Umma wakati anaingia madarakani, wakati awapo madarakani na anapoacha madaraka, alifafanua Mhe. Nsekela.”

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Ibrahim Mipawa alishukuru kwa kupata mafunzo kuhusu Muundo na utendaji kazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

“Nashukuru kwa elimu tuliyoipata kuhusu Muundo wa Taasisi hii. Natoa wito kwa Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu na kuepuka mihemko mnapotekeleza majukumu yenu,” alisema Mhe. Mipawa.

Baraza la Maadili linaundwa kwa Mujibu wa kifungu cha 26(1) kinachosema kuwa “kwa madhumuni ya Sheria hii ya Maadili ya Viongozi wa Umma Baraza litakuwa na watu watatu watakaoteuliwa na Rais, miongoni mwao akiwemo aliyeteuliwa kutoka miongoni mwa watu wenye wadhifa au wamewahi kuwa na wadhifa wa Jaji wa Mahakama Kuu na wengine wawili watachaguliwa kwa ushauri wa Kamishna”.

Kazi ya Baraza la Maadili ni kufanya uchunguzi wa kina kuhusu malalamiko ya ukiukwaji wa masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yaliyowasilishwa mbele yake na Sekretarieti ya Maadili.

Aidha, Baraza litafanya uchunguzi wake hadharani, ila tu linaweza kuwazuia waandishi wa habari, baadhi yao au wote ikiwa linaona kuwa ipo haja ya kufanya hivyo kwa ajili ya kulinda na kudumisha amani, utulivu kwa uendeshaji bora wa mwenendo wa uchunguzi au kwa sababu nyingine yoyote.