Wakuu wa Idara, Vitengo na Makatibu Wasaidizi wa Kanda wa Sekretarieti ya Maadili ‘wapigwa Msasa’ kuhusu Uongozi.


Wakuu wa Idara, Vitengo na Makatibu Wasaidizi wa Kanda wa Sekretarieti ya Maadili ‘wapigwa Msasa’ kuhusu Uongozi.
29
Apr
2020

Wakuu wa Idara, Vitengo na Makatibu Wasaidizi wa Kanda wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ‘wapigwa Msasa’ kuhusu Uongozi.

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela, amewataka watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwa waadilifu katika utekelezaji wa Majukumu yaona kwambauadilifu wao haupaswi kutiliwa mashaka.

MheshimiwaJaji Nsekela ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa wakuu wa Idara, Vitengo na Makatibu Wasaidizi kutoka Kanda zote pamoja na Makao Makuu yaliyofanyika MkoaniMorogoro hivi karibuni.

“Sisi kama taasisi tunapaswa kuwa kioo kwa viongozi tunaowasimamia kwa mujibu wa Sheria ya Maaadili Na. 13 ya mwaka 1995. Uadilifu wetu unatupasa kwanza kujitathmini wenyewe kabla Mamlaka ya nidhamu haijachukua hatua,” alisema.

Kamishna Nsekela aliongeza kuwa, watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na Muundo wa taasisi katika kutoa huduma bora katika jamii.

Aidha, Mhe. Nsekela katika hotuba yake amekemea tabia ya baadhi ya Wakuu wa Idara, Vitengo na Makatibu Wasaidizi ya kuwagawa na kutowaheshimu watumishi walioko chini yao kuacha tabia hiyo mara moja kwasababu haijengi umoja na mshikamano ndani ya Taasisi.

“Katika siku za hivi karibuni kumeibuka tabia kwa baadhi yenu kuwagawa watumishi kwa kuweka tabaka la wanaojua kazi na wasiojua, hivyo inapelekea baadhi ya watumishi kutopangiwa kazi na wengine kurundikiwa kazi. Baadhi yenu hamshushi kazi kwa watumishi mnaowaongoza, kazi zote mnataka kufanya nyinyi hasa zenye posho na zinazoambatana na kusafiri,” alisema.

Kamishna Nsekela aliongeza kuwa, ili kujenga umoja na mshikamano ndani ya taasisi, kila Mkuu wa Idara, Kitengo na Ofisi za Kanda aweke mgawanyo wa majukumu na kumfanya kila mtumishi ashiriki ipasavyo kwenye kazi za taasisi ili kujenga umoja na mshikamano.

Aidha Mhe. Nsekela amewakumbusha washiriki hao wa mafunzo ya uongozi kuepuka mgongano wa maslahi wanapotekeleza majukumu yao.

“Tunatambua madhara ya ukosefu wa maadili kwa watumishi wa umma hasa uwepo wa mgongano wa maslahi kwa viongozi wa umma.Kwa kuzingatia suala hili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ameielekeza taasisi yetu kuhakikisha elimu ya mgongano wa maslahi inatolewa kuanzia ngazi ya kata,” alisema.

Kwa upande wake Bw. Kadari Singo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi alisema, kumekuwepo na changamoto kubwa katika siku za hivi karibuni kutokana na baadhi ya viongozi kutoandaliwa vizuri kushika madaraka.

“Baadhi ya viongozi wanapokuwa madarakani, hawachambui mambo kabla ya kufanya maamuzi.Kiongozi anatakiwa kuchambua mambo na kuwa msaada kwa watu anaowaongoza, Serikali na taasisi anayosimamia sio kupenda kuabudiwa” alisema.