Watumishi wa Maadili watakiwa kujitafakari:


Watumishi wa Maadili watakiwa  kujitafakari:
15
Jun
2020

Watumishi wa Maadili watakiwa kujitafakari:

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Harold Nsekela amewataka Viongozi wa Kanda

na watumishi wengine wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kujitafakari kwa kina katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Mhe. Nsekela alitoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo yaliyohusu 'Risk Management' yaliyofanyika hivi karibuni katika Ofisi ya Kanda ya Mashariki iliyopo Mkoani Morogoro.

Aidha, Mhe. Nsekela katika hotuba yake alisisitiza kuwa kila mtumishi anatakiwa kufanya kazi kwa kufuata miongozo na taratibu za utumishi wa umma na kwamba hatosita kumchukulia hatua za kinidhamu mtumishi yeyote atakayefanya kazi kinyume na miongozo na taratibu za kazi zilizowekwa.

Mhe. Kamishna aliongeza kuwa,hatokuwa tayari kumvumilia kiongozi yeyote wa Kanda husika ambaye hatofuata maagizo na maelekezo yake katika utekelezaji wa majukumu yake ya kazi kwa faida ya Taasisi.

“Sitokubali mimi nitoe miongozo na isitekelezwe. Nitakuchukulia hatua za kinidhamu alisisitiza Mhe. Nsekela”.

Mhe. Nsekela aliongeza kuwa, kwa mtumishi atakayefanya kazi kwa bidii na kufata maelekezo hatosita kumpongeza na atakayefanya kazi kinyume na maagizo hatotoa sifa za uongo pale atakapotakiwa kumuelezea mtumishi husika juu ya utendaji wake wa kazi na kwamba hatokuwa tayari kutoa sifa za makaburini atasema ukweli.

Mhe. Nsekela katika hotuba yake aliongeza kuwa, anapotoa maelekezo na miongozo katika utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi yanatakiwa kufuatwa kwa yule ambaye ataenda kinyume na maelekezo anao uwezo wa kumchukulia hatua ikiwemo kumuondoa katika Taasisi.

Aliongeza kuwa watumishi wa Maadili wanatakiwa kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa Uadilifu mkubwa na kujituma wasiifanye Taasisi hiyo kama Kitega uchumi.

Kuhusu suala la Mafunzo kwa watumishi, Mhe. Nsekela alifafanua kuwa Taasisi haimzuii mtumishi yeyote kujiendeleza kimasomo bali mtumishi anatakiwa kuomba mafunzo kwa kufuata taratibu na miongozo ya Utumishi wa Umma ambayo imewekwa kwenye 'Standing order'.

Mafunzo hayo ya Viatarishi yalishirikisha Makatibu Wasaidizi wa Kanda zote pamoja na baadhi ya Maafisa wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoka Kanda mbali mbali pamoja na Makao Makuu.