Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji ( EWURA) watakiwa kuzingatia misingi ya maadili.


Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji ( EWURA)  watakiwa kuzingatia misingi ya  maadili.
26
Jul
2022

Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati na Maji ( EWURA ) wametakiwa kuzingatia misingi ya Maadili katika sekta ya Umma ili kulinda maslahi ya Umma na kukuza Uwajibikaji kwa umma katika utekelezaji wa Majukumu yao ya kila siku.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati- Dodoma Bi Jasmin Awadh katika mafunzo kuhusu maadili kwa watumishi hao.

Bi. Jasmin alifafanua kuwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria ya Utumishi wa Umma pamoja na kanuni zake zimeainisha baadhi ya misingi ya maadili inayopaswa kuzingatiwa ambayo ni Uadilifu, Uwazi, Uwajibikaji , Uaminifu na ukweli, matumizi sahihi ya taarifa , kuepuka mgongano wa maslahi, kutenda haki na kutopendelea, Kuheshimu Sheria pamoja na kutokupokea zawadi .

Bi. Jasmin aliendelea kuelezea kusema kuwa watumishi wa Umma pamoja na Viongozi wa Umma wanatakiwa kuwa na huruma, kuwa wasikivu , wanapotekeleza majukumu yao kujitolea kusaidia wengine kuwa natabia na mienendo mema inayokubalika katika jamii,kuwa mnyenyekevu, kujizuia na tama,kuwa tayari kukubali kukosolewa kufikiri kwa makini kbla ya kutenda pamoja na mengine mengi yenye maadili mema.

Bi Jasmin alieleza kuwa endapo watumishi na Viongozi wa Umma watazingatia misingi hiyo ya maadili itasaidia serikali kupata matokeo chanya katika kila idara na wananchi kuwa na imani na serikali yao kwani watumishi wanafanya kazi kwa niaba ya serikali.

Aidha Bi.Jasmin aliongeza kuwa watumishi wa Umma na Viongozi wa Umma wanapaswa kuzingatia maaadili kwa kiwango cha juu kwani maadili ni kinga ya maovu yote .’’Yatupasa kila wakati kupima faida na madhara ya matendo yetu na kuamua kutenda jambo sahihi wakati wote’’ alisema.

Pamoja na hayo Bi. Jasmin alibainisha kuwa watumishi wa umma pamoja na viongozi wa umma wanapokua waadilifu husaidia kupungua kwa makosa ya rushwa na makosa mengine. Hivyo basi kila kiongozi na mtumishi wa Umma anapaswa kuwa muadilifu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. ‘’Uadilifu unaanza ndani ya nafsi yako mwenyewe huwezi kutoa kitu ambacho huna’’alisema.

Ni wajibu wa kila Kiongozi na kila mtumishi wa Umma kukuza na kudumisha uadilifu na kulinda rasilimali za Umma nchi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Taifa.