Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili wafanya ziara Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)


Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili wafanya ziara Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
21
Aug
2020

Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili wafanya ziara Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)

Baadhi ya Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili wamefanya ziara ya kujifunza katika Ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kujifunza namna vipindi vinavyozalishwa na kurushwa hewani ikiwa ni sehemu ya mafunzo ya siku tano kuhusu Mawasiliano kupitia vyombo vya habari na stadi za uwasilishaji wa mada kuhusu mgongano wa maslahi yaliyofanyika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Katibu, Idara ya Ukuzaji wa Maadili Bw. Waziri Kipacha alisema kuwa Shirika la Utangazaji Tanzania ni wadau wao wakubwa katika suala zima la kukuza na kuhamasisha maadili nchini.

Bw. Kipacha aliendelea kubainisha kuwa kwa kipindi cha muda mrefu wamekuwa wakilitumia shirika hilo kurusha vipindi vya redio kupitia TBC Taifa pamoja na kuhudhuria mialiko mbalimbali ya kituo cha TBC 1 kushiriki katika vipindi vilivyokuwa na maudhui ya Maadili.

Akijibu swali la Waandishi wa Habari kuhusu hali ya Maadili nchini katika kipindi cha miaka mitano, Bw. Kipacha alisema kuwa kwa kutumia kigezo cha urejeshaji wa Matamko ya Rasilimali na Madeni kiwango cha urejeshaji wa matamko kimepanda kutoka asilimia 70 mpaka asilimia 95 na kuendelea.

Pia, akitumia kigezo cha kupokea malalamiko yaliyohusu ukiukwaji wa maadili Bw. Kipacha alisema kuwa katika kipindi hicho cha miaka mitano malalamiko ya ukiukwaji wa maadili yamepungua kwa kiasi kikubwa hali inayodhihirisha kwamba kiwango cha uadilifu miongoni mwa viongozi wa umma nchini imeimarika.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania Dkt. Ayubu Ryoba alisema kuwa suala la maadili wanalichukulia kwa uzito mkubwa katika shirika lake.

Kwa mujibu wa Dkt. Ryobaaliongeza kuwa Maadili ni maadili tu, hata katika vyombo vya habari hususani shirika lake wanalichukulia kwa uzito mkubwa ikiwa ni pamoja na kufuatilia kwa kina na kufichua baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo utekelezaji wake imeonekana kuwa na viashiria vya kukosekana kwa maadili.

Sekretarieti ya Maadili iliandaa mafunzo ya siku tano yaliyoanza tarehe 17-21 Agosti, 2020 yaliyohusu Mawasiliano kupitia Vyombo vya Habari na Stadi za Uwasilishaji wa Mada kuhusu Mgongano wa Maslahi yaliyoendeshwa na Wakufunzi kutoka Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kufanyika katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania jijini Dar es Salaam.