Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili wajengewa uwezo katika Mawasiliano na Stadi za Uwasiliashaji wa Mada.


Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili wajengewa uwezo katika Mawasiliano  na Stadi za Uwasiliashaji wa Mada.
18
Aug
2020

Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili wajengewa uwezo katika Mawasiliano kupitia Vyombo vya Habari na Stadi za Uwasiliashaji wa Mada kuhusu Mgongano wa Maslahi.

Sekretarieti ya Maadili imeandaa mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo Watumishi wake kutoka Ofisi za Makao Makuu na Ofisi zake za Kanda nane kuhusu Mawasiliano kupitia Vyombo vya Habari na Stadi za Uwasilishaji wa Mada kuhusu Mgongano wa Maslahi.

Mafunzo hayo ya siku tano yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu Huria Tanzania tarehe 17 Agosti, 2020 jijini Dar es Salaam.

Akifungua Mafunzo hayo, Kamishna wa Maadili Mhe. Harold Nsekela alisema kuwa kusudi kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watumishi wa Sekretarieti ya Maadili namna ya kuwasiliana kupitia vyombo vya habari na ustadi wa kuwasilisha mada kuhusu mgongano wa Maslahi.

“Mawasiliano ni njia muhimu katika kufikisha ujumbe kuhusu mgongano wa maslahi.Kukosa ujuzi na umahiri katika kuzungumza au kuwasiliana vizuri hata kwa mtu mmoja tu katika jamii kunaweza kushusha heshima na kuaminika kwa Taasisi pamoja na kutoelewaka kwa ujumbe wenyewe ambao ulikusudiwa kuwasilishwa” alifafanua Mhe. Nsekela.

Mhe. Nsekela aliendelea kubainisha kuwa Ukamilifu wa mawasiliano unatimia pale ambapo wapokeaji wa ujumbe husika wameelewa ni nini muwasilishaji alikusudia kusema na kwamba unaweza kupoteza muda na rasilimali fedha bure kama ujumbe ulioukusudia hautoeleweka kwa walengwa.

Kuhusu usimamizi wa suala la Mgongano wa Maslahi, Mhe. Nsekela alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili imeandaa Kanuni za Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma zinazohusu udhibiti wa mgongano wa Maslahi.

Kwa mujibu wa Mhe. Nsekela, Kanuni hizo zimechapishwa katika Gazeti la Serikali kupitia Tangazo Namba 113 la tarehe 14/2/2020 na kusisitiza kuwa ni vyema viongozi na wananchi wakawa na uelewa wa kutosha kuhusu masharti hayo ya nyongeza ya Sheria.

Sambamba na hayo, Mhe. Nsekela alitumia fursa hiyo kuwahasa watumishi wa Sekretarieti ya Maadili kuifahamu Sekretarieti ya Maadili na Kanuni zake hususani Kanuni zinazohusu udhibiti wa Mgongano wa maslahi.

“Sisi wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili tunalazimika kuifahamu kwa kina Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Kanuni zake hususani za udhibiti wa mgongano wa maslahi vyenginevyo tutakuwa wababaishaji kitu ambacho sio kizuri.Lazima tuwe na uhakika wa mambo ambayo tunaenda kuyafundisha ili kuepuka sio tu kujipa aibu wewe binafsi bali kuiaibisha Taasisi” alisisitiza Mhe. Nsekela.

Mafunzo hayo ya siku tano yaliyoanza kuanzia tarehe 17 -23 Agosti, 2020 yaliendesha na Wawezeshaji kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Shule Kuu ya Uhandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma.